MWENDESHA BAISKELI AMUOMBA RAIS SAMIA SIKU YA KIFO CHA MAGUFULI KUWA YA MAPUMZIKO
................
Na Dotto Mwaibale, Singidani Blog
Mwendesha Baiskeli John Augustino Shayo ambaye yupo safarini kuelekea Chato
akitokea Dar es Salaam ameendelea kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuifanya
siku ya kumbukizi ya kifo cha Hayati Rais wa Awamu ya tano Dkt. John Pombe
Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021 iwe ya mapumziko.
Shayo akizungumza na waandishi wa habari mkoani Singida wakati akiwa katika
safari yake hiyo ya kuhamasisha umoja, mshikamano, amani na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya
kumuenzi Hayati Rais John Magufuli alisema pamoja na uhamasishaji huo lengo
lake kubwa ni kwenda kujumuika na familia ya Magufuli katika kilele cha
maadhimisho ya miaka mitatu ya kifo chake na kupeleka ujumbe huo wa kumuomba
Rais Samia kuifanya siku hiyo kuwa ni ya mapumziko kwa kuzingatia kuwa Hayati
Magufuli ni Rais wa kwanza hapa nchini kufariki akiwa madarakani.
“Maono yangu ya kusafiri kwa kuendesha baiskeli kwenda Chato kwa ajili ya
kuhamasisha jambo ili na kumuomba Rais Samia kuifanya siku hiyo kuwa ya
mapumziko niliyapa tangu mwaka jana lakini nilishindwa kufanya hivyo kutokana
na mambo kadhaa yaliyokuwa nje ya uwezo wangu zikiwepo fedha za kujikimu nikiwa
safarini,” alisema Shayo.
Shayo aliwashukuru watanzania ambao wamemuwezesha kumsaidia kwa namna moja
au nyingine kwa kufanikisha safari hiyo ambapo ameendelea kuwaomba waendelee
kufanya hivyo ili aweze kupata maji, chakula, biskuti na glukosi na mahitaji
mengine akiwa safarini.
Aidha, Shayo amewataka vijana waendesha baiskeli wa Igunga, Shinyanga,
Mwanza, Geita, Katolo na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa watakao kuwa tayari
kuungana naye kuelekea Chato kwa ajili ya uhamasishaji huo wawasiliane naye ili
waweze kupanga eneo la kukutana.
Shayo alitumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania watakao kuwa tayari kumsaidia kwa fedha ya chakula wakati akiwa safari wanaweza kumtumia kupitia namba ya simu 0789-060614 pia wanaweza kumtumia ujumbe mfupi wa njia ya simu kwa mawasiliano zaidi.
---ANGALIA VIDEO CHINI---
No comments