Breaking News

WANAHABARI SINGIDA WALIA KUTO SHIRIKISHWA KURIPOTI HABARI ZA OFISI YA MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego.
Baadhi ya waandishi wa habari Mkoa wa Singida wakiwa kwenye majukumu yao ya kikazi.

..............................................

Na Mwandishi Maalumu

WAKATI Tanzania ikitajwa kuwa ni kinara kwa Uhuru wa vyombo vya Habari baadhi ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida wamesikitishwa na utaratibu mbovu wa Kitengo cha Habari kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kuwabagua na kuwatumia baadhi ya waandishi hao hao kila siku kwenda kuandika taarifa za mkuu wa mkoa licha ya kuwepo kwa waandishi zaidi ya 30 wa vyombo mbalimbali mkoani humo.

Kibaya zaidi baadhi ya waandishi wanaotumiwa kuripoti taarifa za mkuu wa mkoa ni wale waliokuwa wakipiga picha mitaani jambo ambalo ni kuidharau Tasnia ya Habari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti waandishi hao wamemtaja Kaimu Afisa Habari Mkoa wa Singida kwamba ni changamoto kubwa na kuwa wahusika  wanapaswa kuchukua hatua za makusudi kuifanyia kazi mapema changamoto hiyo ili Mkoa wa Singida uweze kutangazwa vizuri mafanikio yake kupitia kazi zinazofanywa na mkuu wa mkoa na Taasisi nyingine za Serikali.

Wamesema Kitengo cha Habari Mkoa wa Singida kimekuwa kikiwatumia wapiga picha hao ili kulinda maslahi yao kutokana na kuwamudu huku wakiwahofia waandishi wenye Taaluma kutokana na Kaimu Afisa habari huyo kutokuwa mwanataaluma na hana uwezo wa kuandika habari ambazo zinawekwa kwenye mtandao wa ofisi hiyo (Website).

Waandishi hao ambao wanapewa kipaumbele katika ziara hizo ni wale wanaomsaidia kaimu afisa habari huyo kutengeneza clip za video na kumuandikia habari.

Rais Samia Suluhu Hassani amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inapaswa kufahamika kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na si waandishi hao wasio zidi wanne tena peke yao kila siku ambao wamefikia hatua ya kuitwa waandishi wa mkuu wa mkoa.

Waandishi hao wamehoji kuwa kama hofu ni posho kwa ajili ya bando basi ofisi hiyo iweke utaratibu wa ratiba za kupokezana kwa waandishi katika ziara mbalimbali za mkuu wa mkoa na idara nyingine za Serikali badala ya kuwatumia waandishi anaowataka kaimu ofisa habari huyo.

Kuendelea kukaa kimya na kutochukua hatua kwa ofisi ya mkuu wa mkoa ya kumleta Afisa Habari wa Mkoa kutaendelea kufifisha kutangaza mafanikio ya Serikali kupitia vyombo hivyo vya habari.

Wanahabari hao wamesema kwa mara kadhaa wamewaomba wasaidizi wa mkuu wa mkoa nafasi ya kukutana na mkuu wa mkoa ili kueleza kero hiyo lakini juhudi zimeonekana kugonga mwamba.

Jambo hili halipo ofisi ya mkuu wa mkoa pekee bali lipo hata kwenye taasisi zingine za Serikali zikiwemo Halmashauri za Wilaya ambazo nazo zimekuwa zikiwatumia baadhi ya waandishi.

Katika Halmashauri hizo waratibu wa vikao vya mabaraza ya madiwani wametajwa kuwa na waandishi wao ambao kila mabaraza hayo yanapofanyika huwa wanawaita hao hao pasipo kufanya mizania ya kuwabadilisha jambo ambalo linaonesha kuwepo kwa kitu nyuma ya pazia ikiwezekana Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Singida ifanye uchunguzi wa jambo hilo.

Ikumbukwe kwamba ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia mkuu wa mkoa husika ndio chanzo kikuu cha taarifa mbalimbali za Serikali na taasisi zake.

Hali hiyo imekwenda mbali zaidi hadi kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya zake ambako nako wanafanya hivyo katika kila ziara zao za kikazi na hata wanapokuja viongozi wa juu wa chama hicho mkoani hapa nao wanawaandishi wao wanaowatumia bila ya kuweka utaratibu wa kupokezana na kuonesha kuwa huenda kitengo cha Itikadi na uenezi ndio chenye changamoto hiyo ya kushindwa kuratibu vizuri suala la waandishi katika ziara hizo.

Kutokana na utaratibu mbovu wa kitengo hicho cha habari hata wanapofika Mawaziri kutoka wizara mbalimbali kwenye ziara zao za kikazi mkoani hapa waandishi wanaokwenda nao kwenye ziara hizo wanakuwa ni walewale ambao wamekuwa wakitumiwa na kaimu huyo wa kitengo hicho cha habari..

“Waziri anakuja kukagua miradi inayotekelezwa na Serikali kwa gharama kubwa eti anakwenda na waandishi wawili tu hiyo haileti maana kabisa kwani ni vigumu wananchi kuielewa,” alihoji mmoja wa waandishi hao.

Waandishi hao wanamuomba mkuu mpya wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ambaye anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani katika mambo yote ya maendeleo na kufikisha ujumbe wa Serikali kwa wananchi kulifanyia kazi jambo hilo ambalo kama litanyamaziwa mafanikio ya Serikali katika nyanja mbalimbali mkoani hapa yatashindwa kueleweka kwa wananchi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais utakaofanyika mwakani 2025.

Malalamiko ya namna hii hayapo kwa Mkoa wa Singida pekee bali na mikoa mingine kutokana na mifumo waliyojiwekea baadhi ya maafisa habari na taasisi zingine za Serikali yakiwemo mashirika ya umma.

No comments