EWURA YARAHISISHA MASHARTI VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI
..................................
Na Mwandishi Wetu-Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahamasisha wafanyabiashara wa mafuta
kuwekeza vituo vya bidhaa hiyo maeneo ya vijijini kwa kuwa imerahisisha
masharti ya ujenzi wa vituo hivyo hali itakayosaidia kukomesha uuzaji holela wa
bidhaa hiyo kwenye vidumu na maeneo yasiyo rasmi unaweza kusababisha milipuko
na kusababisha maafa hivyo kuweza kukidhi viwango vya usalama, utunzaji wa
mazingira, mali na watu.
Mkaguzi Mkuu wa mafuta,
EWURA Kanda ya Kati, Arthur Lyatuu, alisema hayo kwenye maonesho ya wakulima
yanayofanyika viwanja vya Nzuguni, Dodoma .
"Tunajitahidi kuhamasisha watu wajenge
vituo vya mafuta ili kuimarisha huduma hii kule vijijini kwasababu maeneo hayo
bado yba vituo vituo vichache na uhitaji wa bidhaa za mafuta umeendelea
kuongezeka, hivyo vituo hivi vitasaidia kuondoa hatari iliyopo sasa ya watu
kufanya biashara hiyo kwa kificho na maeneo hatarishi"alisema
Lyatuu ameeleza zaidi kuwa,
wapo wananchi wanaofanya biashara hiyo kiholela na EWURA inapowabaini imekuwa
ikiwashauri kufungua kituo kidogo cha mafuta ili kufanya biashara hiyo kwa njia
salama kuliko kuweka kwenye madumu makubwa ambayo yanaweza kuleta mlipuko
kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara makubwa ikiwamo vifo na uharibifu
wa mali huku ikiwa pia ni kinyume cha sheria.
Lyatuu, alisema mafuta yanapokuwa kwenye
matenki ya chini ya ardhi siyo rahisi kulipuka kwakuwa yanakuwa salama sana.
Kadhalika alisema ili
kuhamasisha uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini EWURA,
imelegeza masharti ili kuongeza wigo wa huduma.
"Mtu ambaye anataka kuwekeza kituo cha
mafuta kijijini Mamlaka imelegeza masharti ambapo maombi ya kibali cha ujenzi
wa kituo kijijini ni shilingi 50,000 tu, gharama za maombi ya leseni pia
shilingi 50,000/ na leseni shilingi 100,000/ inayolipwa mara moja kwa miaka
mitano ambapo awali ilikuwa gharama sawa kwa maeneo yote"alisema.
Vile vile, alisema masharti
ya tathmini ya usalama wa mazingira ya eneo la ujenzi wa kituo cha mafuta
kijijini ni tofauti na ilivyo mjini.
Mjini lazima Baraza la usimamizi wa mazingira (NEMC) wafanye tathmini lakini kijijini ukaguzi unafanywa na halmashauri husika na muombaji kuandikiwa barua na Mkurugenzi wa halmashauri.
No comments