MRADI WA KUPAMBANA NA MALARIA WA $43 MILIONI WALETA MAFANIKIO NCHINI
.............................................
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
USAID ilitangaza hitimisho ya miaka minne
ya Mradi wa Udhibiti wa Vimelea vinavyosababisha Ugonjwa wa Malaria kupitia
Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI) uliochangia kwa kiasi
kikubwa mafanikio katika mapambano dhidi ya malaria nchini Tanzania.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi huu, zaidi ya vyandarua milioni 20
vyenye dawa ya kuua mbu waenezao ugonjwa wa malaria vimesambazwa katika
Tanzania Bara na Zanzibar, vikiwalinda zaidi ya watu milioni 35. PMI kupitia
USAID ilitoa vyandarua hivyo kupitia kampeni za umma katika shule za msingi na
vituo vya afya, kwa kuzingatia makundi yaliyo hatarini zaidi ikiwa ni pamoja na
watoto wachanga na wanawake wajawazito.
"Ushirikiano wa Marekani na Tanzania umedumu kwa zaidi ya miongo sita,
na tangu mwaka 2006, PMI imewekeza zaidi ya dola milioni 747 kupambana na
malaria nchini Tanzania," alisema Craig Hart, Mkurugenzi wa USAID nchini
Tanzania. "Tunajivunia mafanikio ya Mradi wa Udhibiti wa vimelea
vinavyosababisha ugonjwa wa malaria wa PMI. Ingawa mradi huu maalum
umemalizika, dhamira yetu ya kushirikiana na watu wa Tanzania na kushughulikia
malaria na changamoto nyingine za afya ya umma bado haijabadilika."
Kati ya mwaka 2020 na 2024, mradi huu wa dola milioni 43, ukiongozwa na
Kituo cha Programu za Mawasiliano cha Johns Hopkins kwa kushirikiana na
Tropical Health LLP na Viamo PBC, uliunga mkono juhudi za kulinda asilimia 90
ya watu walioko hatarini. Hii ilijumuisha mikoa 14 yenye maambukizi ya juu ya
malaria, Tanzania Bara na mikoa yote mitano ya Zanzibar, ikiwa ni jumla ya
asilimia 57 ya idadi ya watu nchini Tanzania.
No comments