TANGA URITHI FESTIVAL YAKA NA UCHUMI WA BULUU
Tanga Urithi Festival yaja na Uchumi wa 'buluu,' fursa bwerere kwa Wawekezaji.
Balozi wa Japani nchini Tanzania akaribishwa Tanga kunywa Chai ya Nazi.
Dua ya kumuombea Rais kufanyika Tanga Urithi Festival, pia utakuwepo mdahalo wa Kumbukizi ya Shaban Robert, magwiji lugha ya Kiswahili kukutana.
Majadiliano kuhusu tamasha hilo yakiendelea.
.....................................
Mashaka Kibaya, Tanga
BALOZI wa
Japani nchini Tanzania na familia yake ni miongoni mwa wageni wanaotarajiwa
kunogesha tamasha la Tanga Urithi Festival linalotarajiwa kufanyika katika
Halmashauri ya Jiji la Tanga kuanzia Disemba 27 mwaka huu na kutamatishwa
Januari Mosi.
Taarifa hiyo
imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Salha Burian katika Mkutano
wake na Waandishi wa Habari akisema, Disemba 28 Balozi wa Japani na wageni
wengine watapata fursa ya kuonja Chai mbalimbali zinazotumiwa na Wakazi wa Mkoa
wa Tanga.
"Tarehe
28 itakuwa Uchumi wa buluu kwenye ratiba yetu, Balozi wa Japani atakuja na familia
yake na kutakuwa 'Tea Party' ambapo Balozi na wageni wengine watapata fursa
kuonja Chai mbalimbali tunazotumia kama Chai ya Nazi,nanasi, Chai ya pilipili
na alkasusi"alisema RC Tanga.
Tanga Urithi
Festival pia itatoa fursa ya kufanyika kwa Dua ya kumuombea Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan na Watanzania wote huku kukitarajiwa kufanyika kwa mdahalo wa
Kumbukizi ya nguli wa lugha ya Kiswahili Marehemu Shaban Robert.
Kupitia
Mkutano wake huo na wanahabari,RC Balozi Dkt Batilda Salha Burian
amewakaribisha watu wote kushiriki tamasha hilo,akisema Wawekezaji wanaweza
kuja Tanga kama eneo mojawapo la kimkakati.
Amesema, kwa
kuja Tanga wanaweza kuona fursa kwenye Uchumi wa buluu,uchimbaji wa madini ya
Vito na yale ya viwandani,fursa katika uwekezaji nyumba za makazi,hoteli za
ngazi mbalimbali,uwekezaji kwenye elimu,maeneo ya biashara na hata yale ya
michezo.
Pia tamasha
litatoa fursa kwa Vijana na watu kutoka makundi maalum wenye mawazo mazuri ya
biashara huku wakishindwa kuyaendeleza
ambapo watawezeshwa hatua ambayo itawasaidia katika kukimarisha kiuchumi.
"Wote wanaopenda utamaduni asilia wanapaswa kushiriki, Wajasiriamali na Wawekezaji wanaotafuta fursa wanapaswa kushiriki,watu wa uvumbuzi na wengine wote" alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda.
Taarifa ya
Mkuu wa Mkoa iliendelea kueleza kuwa,tamasha la Tanga Urithi Festival
litahusisha urithi wa chakula,burudani,michezo ambapo pia kutakuwa na Usiku wa
Kanga za kale na burudani asilia zitakayochagizwa na taarabu.
"Kutakuwa
na Usiku wa alwatani,usiku wa mvuvi huku mavazi mbalimbali yakipamba siku hiyo,
mavazi ya Kanga,baibui,msuli na baraghashia kwa Wanaume na mavazi mengine
asilia"alisema Mkuu wa Mkoa.
Mkuu huyo wa
Mkoa alisema, tayari watu kutoka Zanzibar wamekuja na rasmi na taarabu yenye Vifaa
na Zana za kitamaduni huku kukitarajiwa kuwa na Ngoma asilia kama Mdumange na
nyingine kutoka Mkoani hapo.
"Pia
kutakuwa na michezo kama vile bao na mingine mingi kutoka Mwambao wa
Pwani,chakula cha Mwambao,nyama choma,Samaki nk"alisema Mkuu wa Mkoa wa
Tanga.
Pamoja na
hayo,Balozi Dkt Batilda kutakuwa na siku huru kwa ajili ya watu wote kwenda
kutembelea utalii likiwemo eneo la Marine Park ya Samaki aina ya Silikanti.
No comments