TMA YATOA USHAURI KWA WANAHABARI KUHUSU MVUA ZA MASIKA
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang'a ,akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika zitakazoanza Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka wakati akizungumza na waandishi wa habari.jijini Dar es Salaam, Januari 23, 2025.
..............................................
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa ushauri kwa Waandishi wa Habari ili kukabiliana na matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa yatakayoweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.
Ushauri huo umetolewa Januari 23, 2025 jijini, Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang'a wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika zitakazoanza Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka kwa waandishi wa habari.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa Vyombo vya Habari alisema wanashauriwa kufuatilia na kupata taarifa sahihi za utabiri wa Hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kutoa taarifa kwa wakati kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu athari zinazoweza kujitokeza.
“Wanahabari wanashauriwa kutafuta na kutumia ushauri wa kisekta kutoka kwa wataalam wa sekta husika ili kuandaa na kusambaza makala na ripoti za kisekta kwa lugha rahisi kwa lengo la kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya utabiri wa hali ya hewa katika kukabiliana na athari zinazotarajiwa, “ alisema Chang’a.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika.
Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.
Kwa Mawasiliano ya kutoa taarifa zozote zitakazohusu athari kutokana na mvua hizo katika maeneo mbalimbali zielekezwe kwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Chuo Kikuu cha Dodoma,Jengo la Utawala, Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu, 1 Mtaa wa CIVE, S.L.P 27, 41218 Dodoma; Simu: +255 26 2962610: Nukushi: +255 26 2962610 Barua pepe; met@meteo.go.tz; Tovuti: www.meteo.go.tz
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
No comments