Breaking News

MAHAKAMA YA TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA HAKI

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam yaliyofanyika Februari 3, 2025 katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam akizungumza jambo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salma Mussa Maghimbi, aliyeongoza maadhimisho hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam yaliyofanyika Februari 3, 2025 katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salma Mussa Maghimbi, aliyeongoza maadhimisho hayo.

.......................... 

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam 

MAHAKAMA ya Tanzania inaendelea kuimarisha upatikanaji wa haki kwa kuja na maboresho na mikakati kabambe kuelekea Dira ya Taifa 2050. 

 Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salma Mussa Maghimbi wakati akisoma hutuba yake kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika Februari 3, 2025 katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam. 

Alitaja baadhi ya uimarishaji huo ni pamoja na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi wote, hasa wanaoishi vijijini, kwa kuendelea kuboresha miundombinu hususani Mahakama za mwanzo, na matumizi ya mifumo ya kielektroniki ili kufikia watu ambao hawana huduma ya mahakama.

Alitaja eneo lingine kuwa ni kuimarisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro kwa kuimarisha usuluhishi na upatanishi, hususani migogoro ya biashara na uwekezaji ambapo Mahakama ya Tanzania ilianzisha kituo cha Usuluhishi ngazi ya Mahakama Kuu pamoja na kuzitaka Mahakama zote kuwa na ngazi hiyo kabla ya shauri la madai kusikilizwa kwa njia za kimahakama.

 „ Suala la usuluhishi ni muhimu tukalipa nafasi kubwa katika kwa ngazi zote za Mahakama kwa kuwa linaleta matokeo chanya baina ya pande zote mbili za mgogoro, pia linapunguza gharama pamoja na muda wa kumaliza mashauri kwa wakati na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, pia kuendeleza kuwepo kwa mahusiano mazuri baina ya pande zote mbili” alisema Jaji Maghimbi. 

 Jaji Maghimbi alitaja eneo lingine la uimarishaji ni uboresha sheria, kanuni na taratibu za upatikanaji wa haki, ili kupunguza muda wa mchakato wa upatikanaji wa haki na kutengeneza mifumo thabiti ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha uwajibikaji.

Akizungumzia eneo la kuongeza Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuongeza Ufanisi katika utoaji    huduma za Mahakama alisema ni kuwa na mifumo ya Mahakama inayoaminika na kupatikana, yenye ufanisi, uwazi na usalama kwa watumiaji kwa kuwa  na Mahakama inayotumia teknolojia ya kisasa katika shughuli zake zote na kwa ngazi zote za Mahakama.

Akizungumzia mahakama kuongeza imani ya wananchi alisema ni kuimarisha mifumo ya ushirikishwaji wa wadau kwa kuweka mfumo madhubuti wa kushughulikia mrejesho kutoka kwa wananchi na kuongeza mikakati ya utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za upatikanaji wa haki.

Jaji Mghimbi akizungumzia kuimarisha uwezo wa rasilimali watu alisema ni kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa Mahakama ina watumishi wa kutosha kuendana na mzigo wa kazi kwa kuweka mikakati ya kuongeza motisha kwa watumishi wa Mahakama ili kuongeza tija na ufanisi, kutoa fursa za kujiendeleza kitaaluma na mafunzo endelevu kwa watumishi.

Alisema hayo yote yanafanyika ili kumwezesha mwananchi kuendelea na shughuli zake kwani ilizoeleka kwamba mtu anapokuwa na shauri Mahakamani huacha kazi zake zote na kuhudhuria mahakamani akifuatilia shauri lake lakini kwa sasa anaweza kufuatilia shauri lake akiwa sehemu yoyote inachotakiwa awe sehemu yenye mtandao anaweza kuingia katika Mahakama mtandao kisha akaangalia tarehe ya shauri lake na kile kilichojiri Mahakamani au mwenendo uliokuwepo na uliofikia Mahakamani hili linamwezesha mwananchi kuona uwazi na kuongeza uwajibikaji na weledi.

Jaji Maghimbi akizungumzia Nafasi ya Taasisi Zingine Zinazosimamia Haki Madai katika Kutekeleza Malengo ya Dira 2050 na Nafasi ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Wakili Mkuu wa Serikali katika Kusimamia Haki Madai katika Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 alisema Ofisi hizo mbili ni wadau wakubwa katika kusimamia haki madai na zina wajibu mkubwa kusimamia mashauri yote ya madai yanayofunguliwa na serikali dhidi ya mtu, taasisi au kampuni yoyote au madai yanayofunguliwa na serikali ambapo ofisi hizo huwa pia miongoni mwa wadaawa.

 

Alisema zina majukumu makubwa ya kuhakikisha haki madai zinafikiwa kwa wakati kwa kuishauri serikali kutatua migogoro ya kimadai kwa njia ya suluhu.

 

Alisema katika kutimiza Dira ya Taifa 2050 ni muhimu sana mashauri kusikilizwa kwa njia rahisi na zisizomchukulia muda mwingi mwananchi hivyo kuwepo kwa ofisi hizo mbili zinarahisisha kuhakikisha kuwa serikali haiwi chanzo cha kukwamisha mashauri yuanayoweza kumalizwa kwa muda mfupi tena kwa njia rahisi.


Akizungumzia Kuendesha mashauri ya Madai kwa niaba ya serikali alisema kwakuwa mashauri ya madai wakati mwingine yanahitaji ufundi wa kisheria ofisi hizo mbili zimekuwa zikitumiwa katika mashauri hayo hii inasaidia kutokwama kwa mashauri kwa kutokuwepo kwa wataalamu wa sheria hivyo kuwepo kwa ofisi hizo kunawezesha haki madai kusimamiwa kwa misingi ya kisheria.


Nazipongeza ofisi hizi mbili kwa namna ambavyo wanashirikiana na Mahakama katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati,” alisema Jaji Maghimbi. 

Akizungumzia Nafasi na Mchango wa Mawakili wa Kujitegemea Katika Kusimamia Haki Madai Katika Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 alisema Mawakili wa kujitegemea ni wadau wakubwa sana katika kufikia Dira ya Maendeo 2050 katika haki madai. 

Alisema Mawakili wa Kujitegemea mara nyingi ndio wanaowashauri wananchi kufungua madai, kuandaa nyaraka za kufungua shauri, kufungua shauri, kushauri kusuluhisha mgogoro kwa njia ya suluhu muafaka ndani au nje ya Mahakama. 

” Iwapo Mawakili wa Kujitegemea watatekeleza majukumu yao kwa weledi inawezekana kupunguza mashauri Mahakamani hususani yanayofunguliwa bila kuwepo na dai la msingi.” alisema Jaji Maghimbi. 

Jaji Maghimbi alisema Mawakili wa kujitegemea wanao wajibu mkubwa wa kuwashauri kutumia njia mbalimbali za utatuzi wa migogoro bila kupotosha hili litasaidia sana wananchi kuwa tayari kukubali migogoro yao kumalizwa kwa wakati na kusema kuwa analisema hilo kwa kuwa wakati mwingine wananchi huamini njia moja ya  utatuzi wa migogoro Mahakamani kwa kushauriwa au kuelezwa na hawa wawakilishi wa kisheria. 

Jaji Maghimbi akihitimisha hutuba yake akisisitiza uzingatiaji umuhimu wa upatikanaji wa haki katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Mahakama ya Tanzania na taasisi zote zinazoshiriki katika mnyororo wa utoaji wa haki madai na jinai zina nafasi kubwa kuweka mikakati haina budi kutekelezwa ipasavyo ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa katika sekta zote za kiuchumi na kijamii na kuwa na taifa jumuishi, lenye ustawi, haki, na linalojitegemea kufikia 2050  kwa kutokomeza umaskini wa aina zote, na kujenga taifa lenye uchumi imara, jumuishi, na shindani utakaoboresha maisha ya watu.

Aidha Jaji Maghimbi alikumbusha umma kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo kuwa ni endelevu na itaishi kwa mwaka mzima hivyo mambo mbalimbali yataendelea kufanyika kwa kuzingatia kauli mbiu hiyo.

Jaji Maghimbi ameendelea kuwasihi Majaji, Mahakimu, Waamuzi wote pamoja na Mawakili wa serikali na wale wa kujitegema kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuimarisha imani ya Wananchi kwenye vyombo vya utoaji haki pamoja na utii wa Sheria kwa ujumla ambavyo ndio vitasimamia nchi yenye haki na kufanikisha kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo ni Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Picha ya  pamoja na Waheshimiwa Mahakimu.
Picha ya pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bunge walioudhuria maadhimisho hayo.
Bendi ya Jeshi la Polisi (Brass Band) ikitumbuiza.
Wadau wa Sekta ya Mahakama wakiwa kwenye maadhimisho hayo. Mbele ni Majaji Wastaafu walioudhuria Maadhimisho hayo.
 

No comments