DC SAME AAGIZA KUFUKIA MABAKI YA MASHIMO YA UCHIMBAJI MADINI
Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe Kasilda Mgeni amewaagiza wachimbaji wa madini ya viwandani kuzingatia sheria na taratibu za uchimbaji ikiwemo kurejesha mazingira kama yalivyokuwa awali kabla ya uchimbaji wa madini, kulipa ushuru wa serikali kutoa ajira kwa vijana wazawa pamoja na kurejesha faida kwa jamii kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR)
Ametoa maagizo hayo kwenye mkutano wa wadau wa madini mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika wilayani Same ambapo amesema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uchimbaji wa madini na kusimamiwa na sheria ya madini namba 124 ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 na 2019 ambayo inazungumzia suala zima la uongezaji wa thamani ya madini na biashara ya madini.
"Jitahidini sana kujenga mahusiano mazuri baina yenu na Serikali na wananchi kwa kuzingatia sheria na taratibu za uchimbaji wa madini, kutoa ajira kwa wenyeji wa eneo husika, kulipa ushuru wa serikali, kurejesha faida kwa wananchi (CSR) pamoja na kufukia mashimo kwenye maeneo ambayo mmechimba madini ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa mazingira", alisema Mhe Kasilda.
Pamoja na mambo mengine Mhe Kasilda amewasisitiza wadau wa madini kutoa kutoa fursa za ajira kwa vijana na wakina mama wenyeji katika maeneo ambayo shughuli za uchimbaji wa madini unafanyika kwa lengo la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa wananchi wa wilaya ya Same na Taifa kwa Ujumla.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Abel Madaha, alisema lengo la mkutano huo ni kuweka maazimio ya pamoja katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wachimbaji wa madini ya viwandani. Alibainisha kuwa mkoani humo kuna zaidi ya wachimbaji 900 wenye leseni, zaidi ya watu 100 wana leseni za utafiti wa madini, na wengine 40 wana leseni za biashara ya madini.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wa madini ya viwandani wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Emmanuel Bwambo, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wachimbaji mkoani humo, alisema sababu kubwa ya kushindwa kufukia mashimo ni bei duni ya madini hayo sokoni ikilinganishwa na gharama kubwa za uchimbaji na ufukiaji, hali inayosababisha hasara kwa wawekezaji.
Katika mkutano huo, wadau walikubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kuweka bei elekezi kwa wachimbaji, wafanyabiashara na wanunuzi kutoka viwandani ili kusaidia kufidia gharama za ufukiaji wa mashimo. Pia walipendekeza kufanyika kwa vikao vya pamoja kati ya wadau wa sekta ya madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Halmashauri ili kutafuta njia rafiki ya utozaji ushuru na tozo mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha kila mdau anafaidika.
Post Comment
No comments