WAZIRI MASAUNI AANZA ZIARA YA KIKAZI NCHINI NORWAY
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Mha.Hamad Masauni, akiwa katika majukumu yake ya kikazi nchini Norway wakati wa ziara yake nchini.
.............................................‎
‎Na Mwandishi Wetu, ‎Norway‎
‎WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Mha.Hamad M.Y Masauni ameanza ziara ya siku tatu jijini Oslo, nchini Norway na kupokelewa na Bi.Tone Tinnes, Balozi wa Norway nchini Tanzania Mei 11, 2025.‎
‎Ziara hiyo imeratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Norway kufutia mwaliko uliotolewa kwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).‎
‎Lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kupata uzoefu kuhusiana na masuala ya Mazingira, namna bora ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kupitia biashara ya Kaboni na teknolojia ya kutenganisha taka katika miji na kuzifanya kuwa fursa na hatimaye kuzaliwa bidhaa na malighafi zingine ikiwemo mbolea, Maji na nishati ya Umeme.‎
‎Katika ziara hiyo Mhe. Masauni atapata fursa ya kukutana na viongozi wa mbalimbali wa Serikali ya Norway akiwepo Waziri wa Hali ya Hewa na Mazingira wa Norway, Bw. Andreas Bjelland Eriksen, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bw.Asmund Aukrust ,Mkurugenzi Mkuu wa Norad Bw. Bard Vegar Solhjell pamoja na kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Maendeleo endelevu ( sustainable Development)katika Wizara ya Mambo ya nchi za Nje ya Norway. Katika Mikutano hiyo Mhe. Masauni pamoja na viongozi hao watapata fursa ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya Mazingira pamoja na ushirikiano katika jitihada ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa manufaa ya pande zote mbili. ‎
‎Aidha , Mhe.Masauni atapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Manispaa ya Oslo, Hafslunf Celsio, pamoja na kampuni ya Equinor.‎
‎Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo umejumuisha Mwakilishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, Mtaalaam kutoka kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na Wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Mha.Hamad M.Y Masauni akishiriki moja ya kikao katika ziara hiyo.
Post Comment
No comments