MAJENGO YA NHC KARIAKOO KUBOMOLEWA
Na Martin Kuhanga
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeeleza kuwa nyumba zake zote zilizoko katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, zitabomolewa na badala yake yatajengwa majengo makubwa na ya kisasa.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah Hamad , ameeleza kusudio hilo Jumatatu Juni 16, 2025, wakati akizungumza na waandishi na Wahariri wa vyombo vya habari, katika eneo la Morocco Square jijini Dar es Salaam.
Hamad amesema, shirika limejiwekea mpango wa kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitatu, nyumba zote za zamani zitabadilishwa kuwa majengo makubwa ya ghorofa, kuanzia ghorofa kumi hadi 15.
"Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, hakuna jengo lolote la zamani la NHC litakaloendelea kuonekana lilivyo bila kufanyiwa mabadiliko na kuwa la kisasa" amesema Hamad.
Mkurugenzi Mkúu huyo wa NHC amesema, katika kutekeleza mpango huo wa kuigeuza Kariakoo, shirika limeanza utekelezaji wa miradi 16 katika eneo hilo kwa sasa.
Amesema, mbali na miradi hiyo iliyoanza kutekelezwa, ipo miradi mingine 64 iliyopo mbioni kutekelezwa katika eneo hilo la Kariakoo na kulifanya eneo hilo kuwa kisasa.
Kuhusu maendeleo ya Shirika, Hamad amesema, pamoja na mambo mengine, katika kipindi cha miaka mitano, 2019/20 hadi 2023/24, mapato ya shirika yamekua kutoka Shilingi Bilioni 125 kwa mwaka hadi Shilingi Bilioni 189, ikiwa na ukuaji wa mapato wa asilimia 34.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHC amesema, shirika litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuendeleza sekta ya nyumba nabmiliki kama ilivyoelekezwa na Marekebisho Mbalimbali ya Sheria (Miscellaneous Amendment Law) 2005 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2025.
No comments