SHINYANGA KUNUFAIKA NA MIRADI YA REA, WAUZIWA KWA RUZUKU MITUNGI 13, 000
Kila wilaya kunufaika na mitungi ya gesi 3,255
REA yachochea ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi
Mradi kupunguza ukataji wa miti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi
REA yachochea ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi
Mradi kupunguza ukataji wa miti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi
Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) umeitambulisha kampuni ya Lake Gas Limited ambayo imepewa jukumu la
kusambaza mitungi ya gesi 13,020 itakayouzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50
katika Mkoa wa Shinyanga.
Hayo yamebainishwa leo Juni 2, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
na Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Bi. Annet Ndyanabo wakati wa uwasilishwaji wa
taarifa ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji mitungi ya gesi yenye ujazo wa
kilo sita mkoani humo.
Mha. Ndyanabo amesema kuwa mitungi ya gesi 13,020 itakayosambazwa mkoani
Shinyanga ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambao
una lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi kufikia asilimia 80 ifikapo
2034.
"Utekelezaji wa mradi huu unaenda sambamba na malengo ya Mkakati wa
Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia (2024-2034) ambao unalenga
kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ya watanzania
wanaotumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034," Amesema Mha. Ndyanabo.
Ameongeza kuwa, lengo la mradi ni kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati
safi ya kupikia kwa kuwawezesha wananchi wengi kumudu gharama za bidhaa za
nishati safi ili kutunza mazingira.
"Mradi huu utapunguza umaskini kwa kuwapa muda zaidi wanawake kushiriki
katika shughuli za kiuchumi pindi wanapotumia mitungi ya gesi kama njia mbadala
ya kupikia badala ya kuni na mkaa," Ameongeza Mha. Ndyanabo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni ameipongeza
REA kwa kuja na mradi huo na kuiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia
wananchi wengi nishati hiyo muhimu.
Naye, Mratibu wa nishati safi kutoka kampuni ya Lake Gas Limited, Bw. Ramadhan
Siasa amesema watatekeleza mradi huo kwa kuzingatia makubaliano ya Mkataba wa
kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili
kuchochea matumizi ya nishati hiyo.
Gharama ya Mradi huo ni shilingi 272,769,000 na wilaya zitakazonufaika ni
pamoja na Wilaya ya Shinyanga, Kishapu, Ushetu na Msalala na kila wilaya
itapata mitungi 3,255.
Post Comment
No comments