RAIS SAMIA ATOA BILIONI NNE UJENZI KIWANDA CHA KUZALISHA NISHATI MBADALA
REA kugharamia ununuzi wa mtambo wa STAMICO
Stamico yapania kusambaza Nishati Safi ya Rafiki Briquettes kila kona

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Taifa la
Madini (STAMICO) leo tarehe 22 Julai, 2025 wamesaini mkataba wenye lengo la
kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha nishati mbadala (Mkaa mbadala wa Rafiki
Briquettes) mkoani Geita ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni
4.5.
Katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ndogo ya REA, Jijini, Dar es Salaam, REA
itatoa jumla ya shilingi bilioni tatu na STAMICO itatoa shilingi bilioni 1.5;
kwa mchanganuo huo, REA itagharamia ununuzi wa mtambo wakati STAMICO italipia
upatikanaji wa kiwanja, ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji wa
mitambo.
Mkataba huo umesainiwa na Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA pamoja
na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.
Mkataba huo utaifanya STAMICO kuwa na viwanda vikubwa vitano vya kuzalisha mkaa
mbadala wa Rafiki Briquettes; viwanda vingine ambavyo vinaendelea na uzalishaji
wa mkaa mbadala vipo wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, Kiwira mkoani Songwe, na
viwanda vingine viwili vipo mkoani Dodoma na Tabora ambapo vipo kwenye hatua za
mwisho za ukamilishwaji kabla kuanza uzalishaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi, Hassan Saidy, amesema kuwa
Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia
unafikia asilimia 80 kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2034.
“Katika kufanikisha lengo hilo, Wakala unatekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo
uwezeshaji katika kuongeza uzalishaji na usambazaji ili kuongeza upatikanaji wa
nishati safi ya kupikia kwa Watu wa vijijini.”
“Utiaji wa saini wa Mkataba huo kati ya REA na STAMICO ni moja wapo ya
utekelezaji wa maagizo ya Mheshiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa Wakala ili kushirikiana na Shirika la Madini la
Taifa kuona namna ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati safi kwa
Wananchi ili waondokane na matumizi ya nishati zisizo safi na salama”. Amesema
Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu REA.
“Ni matumaini yetu kuwa Mkataba huu utaende kuongeza kasi ya upatikaji wa mkaa
mbadala na kwa bei nafuu ikiwa ni mojawapo ya lengo la Mkakati wa Nishati Safi
ya Kupikia. Tunatambua kuwa utunzaji wa mtambo huu ni muhimu sana ili huduma
iliyokusudiwa iendelee kutolewa kwa wakati bila kuathili uchumi wa Wananchi, afya
na pamoja na mazingira kwa ujumla”. Amekaririwa, Mhandisi, Hassan Saidy.
Mhandisi, Saidy ameongeza kuwa Wakala unaendelea kushirikiana na Wadau
mbalimbali ili kuhakikisha Mkakati wa Nishati safi ya kupikia unatimiza malengo
yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji na usambazaji wa mkaa
mbadala, Wakala unaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo usambazi wa
majiko banifu, usambazaji wa majiko ya umeme, usambazaji wa mitungi ya gesi ya
kupikia majumbani (LPG ya kilo 6 na 15); usambazaji wa gesi asilia katika mkoa
wa Lindi na Pwani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia
katika Taasisi za Umma.
Kwa upande wake, Dkt. Venance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO
ameishukuru Serikali kupitia REA kwa mchango huu ambao utasaidia Shirika hilo
kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha wananchi wote wanaachana na nishati
isiyo safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na hivyo kuunga mkono juhudi
za Serikali za kutunza mazingira.
“Hii ajenda ya matumizi ya nishati safi ambayo kinara wake ni Rais wa Awamu ya
Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kumkomboa Mwanamke ili aachane na
nishati isiyo safi na salama. STAMICO tumejipanga kutekeleza maono haya ya
Kiongozi wetu”, amesema Dkt. Mwasse.
Ameongeza kuwa nishati ya Rafiki Briquettes kwa sasa inatumiwa na Jeshi la
Magereza ambapo Magereza yote 129 nchini kote yanatumia nishati hii kama aina
mojawapo ya nishati ya kupikia, vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Taasisi nyingine ni pamoja na vyuo mbalimbali vya mafunzo, shule za msingi na
sekondari, hoteli, migahawa, na sehemu wanazochoma nyama na chipsi.
Dkt. Mwasse amesisitiza kuwa STAMICO itaendelea kutunza mitambo hiyo ili
iendelee kutoa huduma kwa Wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Hassan Saidy , akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ujenzi wa kiwanda hicho.
No comments