SIMBA TERMINAL YAPOKEA MELI KUBWA WL MURON YENYE TANI 6,970 ZA AMONIUM NITRATE
Na Mashaka Kibaya, Tanga
Kampuni ya Simba Supply Chain Solutions Ltd, inayotoa huduma za kiutendaji bandarini kwa viwango vya kimataifa, imepokea meli kubwa ya mizigo WL MURON iliyobeba tani 6,970 za kemikali aina ya ammonium nitrate kutoka Russia, kupitia Bandari ya Tanga.
Meli hiyo ilitia nanga Julai 25, 2025 katika Bandari ya Tanga, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya kampuni hiyo katika kupanua huduma zake na kuwavutia wateja kutoka mataifa mbalimbali kutumia bandari hiyo muhimu ya kibiashara.
Akizungumza kuhusu ujio wa meli hiyo, Meneja wa Simba Terminal, Awadh Massawe, alisema ni mafanikio makubwa yanayoendana na juhudi za Serikali kupitia maboresho yanayoendelea kufanyika bandarini hapo.
“Shehena hii ya ammonium nitrate itatumika nchini katika sekta ya viwanda na migodi, huku sehemu ya mzigo ikielekezwa katika nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),” alisema Massawe.
Alibainisha kuwa Simba Terminal imeendelea kuimarika kwa kuongeza vifaa vya kisasa kama 'forklifts' na 'packing machines' hali ambayo imeongeza kasi na ufanisi wa kushusha na kusambaza mizigo kwa wakati.
“Tumejidhatiti kutoa huduma bora, jambo ambalo limeendelea kuwavutia wateja kutoka mataifa mbalimbali kutumia Bandari ya Tanga. Pia tunashukuru kwa usalama mkubwa uliopo bandarini, unaotuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Massawe, kampuni hiyo inaendelea kuwekeza jijini Tanga kwa kujenga 'godauni la kisasa' litakalokidhi viwango vya kimataifa kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa mbalimbali za wateja.
Aidha, aliahidi kuwa kampuni itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuunga mkono juhudi za kuboresha miundombinu ya bandari, hali itakayochochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.
Tangu kukamilika kwa maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga, meli ya WL MURON ni ya 13 kupokelewa na Simba Supply Chain Solutions Ltd, hatua inayodhihirisha ongezeko la imani kwa huduma zinazotolewa bandarini hapo.
No comments