WAPIGA KURA 37, 655, 559 KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutanio wa Tume na Wazalishaji Maudhui Mtandaoni kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 03 , 2025.
.....................................
Na
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JUMLA
ya wapiga kura 37,655,559 wanatarajia kushirikia katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2025, huku wapiga kura 36,650,932 wakitokea Tanzania Bara na wapiga kura
1,004,627 wakitokea Tanzania Zanzibar.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Kailima Ramadhani
wakati akiwasilisha mada katika mafunzo kwa wanahabari wazalishaji wa maudhui
mitandaoni ambayo yamefanyika leo Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Kailima
aliwataka wazalishaji wa maudhui mitandaoni kutoa taarifa kuhusu mchakato wa uchaguzi
mkuu wa mwaka huu ili wananchi wajue hatua mbalimbali kuelekea uchaguzi huo.
Alisema
kauli mbiu ya uchaguzi wa mwaka huu ni “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga
Kura” na kwamba imelenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya
tarehe 29 Oktoba, 2025 kwa ajili ya kupiga kura.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele akifungua mafunzo hayo aliwahimiza wazalishaji wa maudhui mtandaoni kutumia majukwaa yao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Alisema Tume inatambua mchango mkubwa wa wazalishaji wa maudhui mtandaoni kwanza ikiwa ni daraja la mawasiliano kati ya Tume na wananchi na wadau wengine na pili wakiwa ni wadau wa moja kwa moja wa mchakato wa uchaguzi huo.
Kwa upande wake Meneja
wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka TCRA,
Mhandisi Andrew Kisaka, aliwataka Wazalishaji
wa maudhui mtandaoni kuepuka kuchapisha taarifa zinazoweza kusababisha taharuki
au kuchochea machafuko.
“ Wakati
wa uchaguzi huwa kuna kuwa na changamoto nyingi za kiitikadi za kisiasa na
hivyo kusababisha mivutano ambayo wakati mwingine inatoa matukio mabaya hivyo
waandishi wa habari mnapaswa kuwa wazalendo wakati wa kuchukua taarifa zenu
kwani wakati mwingine huwa zinachochea vurugu badala ya kusaidia” alisema
Aidha, Kisaka
aliwataka watoa mahudhui hao kujiepusha kusambaza uvumi, kutopendelea upande wowote na kuweka ushabiki
kwa chama chochote na kutumia lugha nzuri.Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Kailima Ramadhani, akiwasilisha mada kwenye mkutano huo.
Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, akitoa mada kwenye mkutano huo.
Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
No comments