WAZIRI AWESO, WAKANDARASI KWENYE MPANGO WA KUKAMILISHA MIRADI YA MAJI
Waziri wa Maji Jumaa Aweso amekutana na kufanya kikao na Rais wa Kampuni ya ujenzi ya kikandarasi ya China Civil Construction Corporation (CCECC) Chen Sichang jijini Dar Es salaam lengo likiwa ni kujadili namna bora ya kukamilisha miradi mikubwa ya maji ya kimkakati nchini ambayo inatekelezwa na kampuni hiyo.
Waziri Aweso akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri wametanabaisha mikakati na kutoa muongozo na muelekeo wa Wizara ya Maji juu ya namna bora ya kushirikiana kuendeleza ujenzi wa miradi na kuikamilisha kwa wakati kwa thamani ya fedha.
Aidha Waziri Aweso amesisitiza kuwa miradi hiyo ni muhimu sana kwa wananchi na wana matumaini makubwa kwani maeneo haya yana uhaba mkubwa sana wa upatikanaji wa huduma ya Maji na miradi hii ni ya kimkakati na muhimu sana kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.
Miradi iliyowekewa mikakati ni pamoja na Mradi wa Maji Makonde, Newala mkoani Mtwara, Mradi wa Maji mji wa Songea mkoani Ruvuma, Mradi wa Maji Simiyu, Mradi wa Maji Rorya-Tarime na miradi mingine ikiwa ni mpango wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha miji hii mikubwa nchini inapata huduma ya Maji yakutosheleza.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi Rais wa kampuni hiyo Mr. Chen Sichang amemuhakikishia Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso na Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri kwamba kazi itaendelea kufanyika kwa mikakati iliowekwa na kukubaliana katika kikao hicho na kuahidi kumaliza kazi zote kwa wakati uliopangwa.
No comments