UMOJA WA WAISLAM RAIA WA AFRIKA KUSINI WATOA MSAADA WA VITI MWENDO ZANZIBAR
Na Dotto Mwaibale, Zanzibar
UMOJA wa Wafanyakazi Waislam Raia wa Afrika Kusini
wanaofanya kazi Dubai kwa kushirikiana na Hussein Ramadhani Layya (Maarufu
Msokolo) wametoa msaada wa viti mwendo kwa watoto 50 wenye uhitaji maalumu
katika hafla iliyoandaliwa na Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Msokolo alisema msaada huo uliotolewa ni sehemu ya kuunga mkono
jitihada za Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kuboresha maisha
ya watu wenye ulemavu.
"Tunapotoa msaada huu kwa wenzetu hawa tunapaswa
kukumbuka kuwa sisi sote tuna udhaifu na changamoto zinazoweza kudhoofisha miili yetu
hivyo, tusisahau kuwa hakuna aliye bora kuliko mwingine, maisha yetu yana
thamani, bila kujali hali ya mtu, umri, jinsia au ulemavu,” alisema Msokolo.
Alisema msaada huo unakwenda kutoa faraja kwa walengwa
ambapo aliomba ushirikiano huo wa pamoja uzidi kuendelea baina ya umoja huo na
wananchi kwa ujumla wao.
Aidha, Msokolo alisema kuwa tukio hilo linatuacha na funzo
kubwa kwamba utu, mshikamano na upendo ni silaha kuu za kujenga jamii yenye
uhitaji na ni heshima kubwa.
Aliongeza kuwa kila kiti mwendo kilichotolewa si msaada
pekee, bali ni daraja la matumaini na uthibitisho kwamba kila mtoto ana haki ya
kuishi kwa heshima.
"Maisha ya kila mmoja wetu ni zawadi na thamani yake
haipimwi kwa udhaifu, bali kwa fursa ya kuonyesha upendo na tunapo wakumbatia
wenzetu wenye changamoto, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya utu wetu sote,”
alisema Msokolo .
Aliongeza kwamba msaada
huo ni ishara ya mshikamano wa kimataifa na unaunga mkono maono ya Rais wa
Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata
heshima, nafasi na huduma wanazostahili.
Kwa upande wake Mwakilishi wa umoja huo, Ahmed Kathrada alisema
kwamba utoaji wa msaada huo ni hatua njema ya kuonesha upendo kwa wahitaji
ambao ni jamaa na ndugu zetu ambao ttupo nao katika familia zetu.
"Nilipata hamasa nilipoona ndugu yangu Msokolo
akikabidhi fimbo kwa ndugu zetu wenye changamoto ya uoni hafifu mwaka jana.
Nilipiga simu kwa wenzangu Dubai, na kwa dakika tano tukawa tumepata fedha za
kununua viti mwendo 50. Huu ni mwanzo tu – tutaendelea kuwasaidia watu wenye
uhitaji maalumu Zanzibar." Alisema Kathrada.
Katibu wa Baraza la
Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, akkizungumza wakati wa kukabidhi
msaada huo aliupongeza umoja huo kwa msaada walioutoa na kueleza umegusa nyoyo
za walengwa.
"Mmetuletea faraja kubwa kwa watoto wetu tunawashukuru
sana Umoja wa Wafanyakazi Waislam kutoka Dubai pamoja na ndugu yetu Msokolo, "
alisema Debe.
..................................................
Kuhusu Ulemavu Zanzibar
Takwimu za Ulemavu Zanzibar (Sensa ya 2022):
Idadi ya watu wenye ulemavu: 145,497 (11.4% ya wakazi wote)
Wanaume: 61,375
Wanawake: 84,222
Tafiti za UNICEF zinaonyesha miongoni mwa changamoto zinazowakabili watoto na vijana ni:
Ugumu wa kusikia – 0.8%
Ugumu wa kuongea/kuwasiliana – 1%
Ugumu wa kujitunza – 1.6%
Ugumu wa kutembea – 0.6%
Hussein Ramadhani Layya (Maarufu Msokolo kushoto) akizungumza wakati wa kutoa msaada huo. Wengine ni viongozi wa umoja wa waislam raia wa Afrika Kusini waliowezesha msaada huo.
Viongozi mbalimbali wa Umoja wa Waislam raia wa Afrika Kusini wakiwa katika picha ya pamoja na watoto wenye uhitaji baada ya kuwakabidhi viti mwendo.
Hussein Ramadhani Layya (Maarufu Msokolo mwenye shati jeusi ) akizungumza na wazazi na walezi wa watoto wenye uhitaji wakati wa kuwakabidhi msaada wa viti mwendo.
Mtoto akiwa na kiti mwendo chake baada ya kukabidhiwa.
No comments