TANESCO RUVUMA YAIKABIDHI SOUWASA CHETI KATIKA MAADHIMISHO YA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA 2025
...................................
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea SOUWASA imekabidhiwa cheti cha heshima na sufuria ya kisasa ya kupikia kwa kutumia umeme (pressure cooker) na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja inayoendelea kote nchini kuanzia tarehe 6 hadi 11 Oktoba 2025.
Akizungumza baada ya kupokea zawadi hizo Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA Mhandisi Patrick Kibasa, amelipongeza Shirika hilo kwa kutambua mchango wa SOUWASA kama miongoni mwa wateja wake muhimu, aidha, amesisitiza dhamira ya mamlaka hiyo kuendelea kushirikiana na TANESCO, ikiwemo kulipa bili za umeme kwa wakati kama sehemu ya kuendeleza uhusiano mzuri uliopo.
“TANESCO kwa sasa wanatoa huduma nzuri na tumekuwa tukipata msaada wa haraka pale ambapo changamoto zinapojitokeza, Tunaendelea kufurahia huduma ya umeme inayotolewa."
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Eusebius Mhelela, amesema TANESCO inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya meme kwa kuwa ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira, ameeleza kuwa zawadi ya pressure cooker ni sehemu ya kampeni ya kuhimiza matumizi ya nishati.
Naye Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Alan Njiro, ameipongeza SOUWASA kwa kuwa mteja mzuri wa TANESCO, amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na TANESCO kwa karibu, hali iliyochangia kuipatia tuzo hiyo kama ishara ya kutambua mchango wao katika mafanikio ya shirika.
Utoaji wa zawadi hizo ni mwendelezo wa shughuli mbalimbali za TANESCO Mkoa wa Ruvuma katika Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, inayolenga kuimarisha uhusiano na wateja, kutambua mchango wao na kuhamasisha matumizi ya nishati ya umeme kwa usalama na tija zaidi.
No comments