WAZIRI MKUU AANZA KAZI KWA KISHINDO HOSPITALI YA RUFAA YA DODOMA
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba , akizungumza na mgonjwa baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma leo Novemba 15, 2025.
...........................................
.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Novemba 15, 2025 amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuziagiza hospitali zote nchini zihakikishe wajawazito wanapofika hospitali wahudumiwe kwa haraka ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizaya ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na Hospitali zote nchini ziweke vipaumbele vya kuwa na dawa kulingana na mahitaji ya eneo husika. “ Haipendezi mwananchi kufika hospitali na kupatiwa vipimo vyote kisha anaambiwa dawa akanunue kwingine, kama duka binafsi linaweza kupata dawa hizo, inawezekanaje hospitali za serikali hapati? Naagiza Hospitali zote ziwe na dawa.”
Ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi nje ya hospitali hiyo baada ya kutembelea wananchi waliofika hospitalini hapo kupata huduma mbalimbali za kitabibu ambapo amesisitiza wananchi waendelee kuhudumiwa vizuri kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini vikiwemo vifaa tiba na dawa.
Kadhalika Mheshimiwa Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini zihakikishe zinakuwa na vifaa vya usafi binafsi vya dharura vikiwemo ndoo na beseni katika wodi za wazazi ili viwasaidie akinamama wasiokuwa na vifaa hivyo. “Ujauzito sio suala la dharura vifaa kama ndoo tunapaswa kuwa navyo katika hospitali zetu za serikali.”
Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika uboreshaji wa huduma za afya nchini. Waziri Mkuu akiwa hospitalini hapo, wananchi walimueleza kuwa wanahudumiwa vizuri na kwa uangalizi wa karibu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini zizingatie maelekezo ya kutumia mifumo sahihi ya malipo katika taratibu za kutoa huduma ili kuwezesha Serikali kuendelea kuhudumia wananchi.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo kufuatia kuwepo kwa hospitali ambazo baadhi ya huduma wanapokea malipo kwa njia ya mtandao na nyingine malipo yanapokelewa malipo kwa njia zisizo rasmi.
Dkt. Mwigulu akizungumza na wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ziara katika hospitali hiyo ikifanyika.
Dkt. Mwigulu akizungumza na wagonjwa katika hosp.





.jpg)




No comments