MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA KILWA ATAJA MPANGO KAZI WAKE WA AWALI
Na Dotto Mwaibale
Mwenyekiti Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi ameanza rasmi kazi ya kuwatumikia wananchi na kuweka bayana mpango kazi wake ambao ataanza nao.
Akizungumza Desemba 12, 2025 kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii ambaye alitaka kujua mpango kazi wake ni upi baada ya kupata nafasi hiyo kwa kuchaguliwa kwa kura za kutosha alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hiyo aliyoipata.
“Kwanza kabisa namshuku Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii siwezi kusema ushindi huu ni wa kwangu bali ni wa wananchi ambao nakwenda kuwatumikia baada ya kupigiwa kura na madiwani kutoka kata 23 wakiwepo nane wa viti maalumu na wabunge wawili,” alisema Ngatanda.
Alisema mambo atakayoanza nayo ni kuhahikisha anashauriana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hemed Magaro katika kuongeza zaidi mapato kwa kuibua vyanzo vingine ili kuongeza mapato mengi licha ya kuwepo kwa mapato mazuri katika wilaya hiyo.
Ngatanda alisema anaamini kwa kuongeza zaidi mapato halmashauri hiyo itaweza kutekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia fedha zinazotokana na mapato ya ndani.
" Jambo langu la kwanza nitakaloanza nalo kwa nguvu zangu zote ni ukusanyaji wa mapato ambayo ndiyo injini ya kuendesha halmashauri zetu," alisema Ngatanda.
Aidha, Ngatanda alisema kama muongozo wa ratiba za kazi ulivyo kwa kila siku mbili katika wiki ni siku za kukutana na wananchi siku moja wapo ataweka utaratibu wa kwenda kwenye tarafa kukutana na walimu ili kujua mahitaji zaidi ya wanafunzi kwenye maeneo yao.
Alisema hatua nyingine itakayofuata ni kukutana na wazee wa wilaya nzima ili kuzungumza nao hasa kuhusu chama chao cha CCM na nini maoni yao kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika wilaya yao.
Ngatanda alitaja mkakati mwingine ambao ataendelea nao ni suala zima la mpango wa chakula mashuleni kuona linafanikiwa zaidi kwani mkurugenzi wa halmashauri hiyo alishaanza kulisimamia vizuri.
Alisema mafanikio ya suala hilo yanaonekana na atahakikisha linaendelea kufanikiwa zaidi hasa kwa wanafunzi wa madarasa ya mitihani wa darasa la nne, la saba, kidato cha pili na kidato cha nne.
Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na madiwani wenzake, wabunge na wataalam wa halmashauri hiyo watayafikia makundi yote ya vijana, na makundi maalum kuhakikisha yanapata elimu na kunufaika na mkopo wa asimia 10 ili kuwaimarisha kiuchumi kuanzia mtu mmoja mmoja kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Ngatanda alisema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wote amekuwa akihimiza uzalendo, mshikamano, amani na upendo kwa ustawi wa taifa letu.
Alisema kwa muktadha huo ataendelea kuunga mkono jitihada hizo za Mhe, Rais kwa kuwa bega kwa bega na vijana na makundi mengine kuhakikisha elimu ya uzalendo inaenezwa wilayani humo ili kuwajenga zaidi na kutojihusisha na vitendo ambavyo vinaweza kupoteza amani kwa kufuata mkumbo wa watu wasiyoitakia mema nchi yetu.
“Haya ni mambo ambayo nitaanza nayo kwa kushirikiana na mkurugenzi wetu ambaye ni mchapa kazi kwani juhudi zake za utendaji tumeziona tangu afike kwenye halmashauri yetu na sisi tutaendelea kumpa ushirikiano wa kila namna lengo likiwa ni kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Ngatanda.
Aidha, Ngatanda alisema amejipanga vilivyo kushirikiana na wananchi, madiwani wenzake, wabunge na wataalam wakati wote wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Halmashauri hiyo na kuitekeleza vyema ilani ya CCM ya 2025/ 2030 kwa vitendo.
Alisema hatua hiyo ni kuungamkono jitihada za Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihimiza kufanya kazi kwa bidii ili kujikomboa kiuchumi na kulipeleka mbele zaidi taifa kiuchumi na maendeleo.





.jpg)




No comments