POLISI TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA, ASKARI WAKE ATUNUKIWA TUZO YA BALOZI WA AMANI DUNIANI
Mrakibu wa Polisi (SP) Balozi Dkt. Ezekiel Abernego Kyogo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania, akionesha Tuzo Balozi wa Amani Duniani (AMB) "Peace Ambassador (AMB)" na Greenling Peace Foundation. baada ya kutunukiwa.
.................................................
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
NENO Amani ni neno ambalo limezoeleka sana miongoni mwa
jamii na limekuwa likizungumzwa na kila mtu wakiwemo viongozi wa kisiasa na
dini kutokana na umuhimu wake.
Mahala popote ambapo hapana Amani hapawezi kufanyika jambo
lolote la maendeleo kama tunavyoona nchi nyingi duniani ambazo Amani imetoweka
kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vita za kugombea madaraka na mali.
Kutokana na kutambua umuhimu wa Amani duniani kote kuna
baadhi ya watu wamekuwa wakijitolea au kufanya kazi ya kuhimiza kudumisha Amani
kwani mara nyingi inapokosekana na kuzuka vita au vurugu wanaokuwa kwenye changamoto
kubwa ni watoto na wanawake.
Nchini Tanzania mmoja wa watu ambaye amekuwa akilipigania
Taifa letu liwe na Amani ni Ezekiel Kyogo.
Jina la Ezekiel Kyogo siyo jina jipya hapa nchini kutokana
na kazi kubwa anayoifanya ya kuhubiri Amani,
Ezekiel Kyogo ni Mrakibu wa Polisi (SP) kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania ambaye amepewa
heshima anayostahili kwa kutunukiwa Tuzo Balozi wa Amani Duniani (AMB)
"Peace Ambassador (AMB)" na Greenling Peace Foundation.
Balozi Dkt. Kyogo amethubutu, ameonesha njia na kuliheshimisha Jeshi la Polisi nchini kwa utoaji wa elimu, uhamasishaji utunzaji wa amani na kubeba bendera ya Taifa kimataifa na kwenye majukwaa makubwa duniani.
SP Kyogo anafanyakazi Kamisheni ya Polisi Jamii Kitengo cha
Ushirikishwaji wa jamii na kazi ya kitengo hicho ni kuelimisha jamii mambo mbalimbali
ya amani, uzalendo na usalama ili kuifanya Tanzania kuwa salama.
Tuzo hizo zilitolewa na Mwenyekiti Mwanzilishi wa Greeling Global Peace
Organization Zambia Prof Bishop Kennedy Songwe pamoja na mgeni rasmi wa hafla
ya utoaji wa tuzo hiyo Balozi Prof. Askofu Rejoice Ndalima.
Katika hafla ya kutunuku tuzo hizo iliyofanyika Ukumbi wa
Rungwe Hotel Jijini Dar es Salaam Novemba 29, 2025 , ilihudhuriwa na wageni
waalikwa, wawakilishi wa taasisi mbalimbli, wanaharakati wa amani na viongozi wa
kimataifa.
Kutunukiwa kwa Tuzo hiyo hakukuwa kwa kubahatisha kunatokana
na kazi kubwa anayoifanya kwa makundi mbalimbali ya kutoa elimu ya kuitunza
Amani na mchango wake mkubwa uliotukuka katika Taifa juu ya Amani.
Sehemu kubwa ya kazi yake Balozi Dkt. Ezekiel Kyogo ni
Amani, Amani, Amani ambayo matunda yake yameonekana kwa kutunukiwa tuzo hiyo ya
kipekee ya ubalozi wa Amani Duniani.
SP Balozi Dkt. Ezekiel Kyogo amekuwa na mchango mkubwa
katika Taifa wa kuelimisha jamii kuhusu uzalendo na kuhamasisha Amani na hiyo
ndiyo kazi yake kubwa anayoifanya ndani ya Jeshi la Polisi kwa liwake jua, inyeshe
mvua yeye ni kiguu na njia kwenda kutoa elimu ya kuhamasisha Amani.
Balozi Dkt. Ezekiel Kyogo anasema Tuzo hiyo ya heshima
aliyotunukiwa ni ya pili baada ya kutunukiwa ya kwanza Oktoba 17, 2025 na Mufti
wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally Temeke Jijini Dar es Salaam.
Balozi Dkt. Kyogo anasema
kutokana na majukumu yake ya kazi ya kila
siku ni muelimishaji wa jamii katika masuala ya ulinzi na usalama kwa
ujumla wake.
Anasema katika maisha huwezi
kuvitenganisha vitu vitatu ambavyo ni Usalama, amani na Utulivu na kueleza
kwamba ili kuwepo na utulivu ni lazima kuwepo na usalama, utulivu na ndiyo amani
inapatikana.
“Tumekuwa tukivihubiri mara
kwa mara kwa jamii kwa muktadha wa kuifanya jamii yenyewe kuwa salama dhidi ya
uhalifu lakini kuifanya jamii ya watanzania kuwa salama dhidi ya maadui wa nje
na kuifanya kuwa na uzalendo wa nchi yao kuwa salama na utulivu zaidi,” alisema
Balozi wa Amani Dkt. Kyogo.
Dkt. Kyogo amesema kazi hiyo
wameihubiri katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa sababu wana amini kwamba
amani ikiwepo ndipo maendeleo yanaweza kuwepo, uzalishaji unaweza kuwepo,
shughuli za maendeleo zitakuwepo pasipo kuwa na changamoto yoyote.
Anasema kwa ujumla wake
ustawi wa binadamu unahitaji uwepo wa
amani na siyo vinginevyo
Dkt. Kyogo anasema kutoweka
kwa amani au vurugu anaichukulia kama ni changamoto ya kijamii (Social Probrem)
na ili tatizo liwe la kijamii ni lazima liwe lina mgusa kila mtu na likiwa la
mtu mmoja haliwezi kuwa la kijamii.
“Linapo mgusa kila mtu, kila
sekta na kila mahali linakuwa ni Social Problem na ndiyo maana nikasema kwamba
kutoweka kwa amani kwa kuanzisha vurugu linakuwa tatizo la kijamii kwa sababu
zinamuathiri kila mmoja wakiwemo wazazi, watoto, walezi, wagonjwa waliopo
mahospitali, kundi la watu wasiyojiweza na kuwa vurugu zinapotokea watu hao
wanakwenda wapi,” alisema Dkt. Kyogo.
Dkt. Kyogo anasema
unapotokea uvunjifu wa amani utatuzi wake unatakiwa uwepo ushiriki wa pamoja wananchi,
watu wa makanisa, madhehebu mbalimbali waislamu, wakristo, vijana, wazee
kutokana na unyeti wake wa kumgusa kila mmoja.
Aliongeza kuwa ili Taifa
liwe salama na uwepo ustawi inatakiwa kukaa pamoja na kuangalia tunatoka vipi
kwenye hayo madhira na kwenda kwenye mazingira salama zaidi.
Dkt. Kyogo anasema tangu
aanze kufanya kazi hiyo ya kuhamasisha amani ana zaidi ya miaka mitano na
kueleza kuwa majukumu ya kuhamasisha amani ni ya kila mtu ingawa baadhi ya watu
wanadhani jukumu hilo ni la polisi.
Akizungumzia kutunukiwa tuzo
hiyo anasema kimsingi anajisikia furaha na kutambua kwamba kazi anayoifanya
mchango wake umeonekana na kwamba mbali ya kufurahi ameongezewa jukumu la
kuendelea kuhamasisha amani.
“Ninavyoongea siku hadi siku
kuhusu amani bado naona nawiwa kuhamasisha amani ili Tanzania iwe salama lakini na hata nchi zingine kwa sababu dunia
inapokuwa salama panakuwa mahali sahihi
pa kuishi,” anasema Balozi wa Amani Dkt. Ezekiel Kyogo.
Dkt. Kyogo alitumia nafasi
hiyo kuyaambia makundi ya vijana na mengine kuwa wanapaswa kuitafakari Tanzania
kwa mapana kwamba imejengwa na imetukuza
na kufika hapa tulipo hivyo ni jukumu letu
kuangalia mbinu mbadala na sahihi ya kuiboresha ili twende mbele
zaidi kwa kuitafakari michango yetu ya
kuiwezesha kufika mahali inapopaswa kufika.
“Tunatakiwa kuwa na wazo la
kuona kwamba sisi kama vijana tutafanya nini kuijenga nchi yetu ifike mahali na
kwasabau imefika mahali pazuri hivyo kuna haja ya kuchangia mawazo yetu kusogea
mbele zaidi na kuona jinsi gani ya kuifikisha nchi yetu pale wanapoona
wanapahitaji,” alisema Dkt. Kyogo.
Katika uelimishaji na
uhamasishaji wa amani Balozi Dkt. Kyogo alisema wanalazimika kutumia mbinu
mbalimbali zikiwemo adithi ili waeleweke na moja ya adithi yake ni ya kijana Tuntufye.
“ Siku moja watoto wa kijiji
kimoja walikaa sehemu na kusemezana wapige kura ili kumpata mama ambaye ni
mrembo miongoni mwa mama zao ambapo mtoto aitwaye Isack mama yake aliibuka
kidedea kwa kuwa mrembo katika kijiji hicho.
Baada ya kupigwa kura hizo mtoto
Isack aliinuka na kutembea kwa madaha akijisifia mbele ya wenzake kuwa mama
yake ni mrembo kuliko wakina mama wote pale kijijini.
‘Hapa nazungumzia mapenzi na
uzalendo kumbe hata kama mtu hayupo akizungumziwa kwa mema watu wengine
wanakuwa na furaha na ndiyo maana mama yake Isack alipotajwa kuwa ni mrembo
mtoto wake alijisikia furaha kubwa,” alisema Dkt. Kyogo.
Lakini wakati huohuo watoto
hao walisemezana tena kuwa palipo na mrembo hapakosi kuwepo na mwenye sura
mbaya, hivyo walipiga kura tena ili kumpata mama mwenye sura mbaya hapo kijijini kura hiyo ilimuangukia mama yake
Tuntufye.
Tuntufye baada ya mama yake
kupigiwa kura hiyo moyo wake ulisinyaa, akanung’unika na kuhuzunika. Kumbe kuna
uzalendo kati ya mtoto na mama, mama akiguswa kwa ubaya mtoto anasikia maumivu
hapa nazungumzia maana ya upendo,’alisema Dkt. Kyogo.
Baada ya mama yake kupigiwa
kura hiyo Tuntufye alianza kuondoka kuelekea nyumbani kwao na alipokaribia
karibu na mlango wao alimkuta mama yake akiinua mikono na kumkumbatia huku
akimuuliza kwa nini analia lakini aliinua uso wake kumuangalia mama yake usoni
na kuthibitisha ni kweli alikuwa na sura mbaya.
Tuntufye aliendelea kulia
ndipo mama yake alipomkumbatia kwa upendo na kumuambia sikiliza mwanangu “wakati
ukiwa mdogo tuliishi kwenye nyumba ya majani moto ulishika ile nyumba ukiwa na
miezi miwili mimi mama yako kwa mahaba na upendo wa dhati niliingia ndani kwa
ajili ya kukuokoa ndipo moto uliponiangukia usoni na kuharibu sura yangu”.
Baada ya Tuntufye kujua
sababu ya mama yake kuwa na sura mbaya alitabasamu hakuhuzunika tena.
Balozi wa Amani Dkt. Kyogo
alisema leo hii tungejua Tanzania ilipotutoa na kujengwa kwa jitihada kubwa
tungeipenda na kuitunza amani iliyopo kwa kusemezana wenyewe kwa wenyewe ili
kuiendeleza na ndiyo maana nimezungumzia dhana nzima ya kushirikiana katika
kuijenga amani na nchi yetu ya Tanzania.
“Tanzania inapokuwa na amani
hata sisi wana Usalama tuna kuwa tunafanya kazi vizuri na wakati mwingine
tunaingia kwenye changamoto mbalimbali kwa kuwa tumekula viapo vya kuhakikisha
tunalinda usalama wa raia na mali zao,” alisema Balozi Dkt. Kyogo.
Aidha, Dkt. Kyogo alisema
kila mtanzania ana wajibu wa kuilinda amani iliyopo nchini na hakuna mtu wa
kuachiwa kuitunza.
Balozi Dkt. Ezekiel Kyogo akiwa katika moja ya matukio yake ya uelimishaji wa masuala ya kutunza amani
Mrakibu wa Polisi (SP) Balozi Dkt. Ezekiel Kyogo akitoa elimu kuhusu masuala ya utunzaji wa amani.
Balozi Dkt. Ezekiel Kyogo, akisisitiza jambo wakati wa utoaji wa elimu kuhamasisha jamii kutunza amani ya nchi.
Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990











.jpg)




No comments