RC TANGA AONYA WENYE NIA YA KUCHOMA MATAIRI BARABARANI KUSHEREHEKEA MWAKA MPYA
.......................................
Na Mashaka Kibaya, Tanga,
MKUU wa Mkoa wa Tanga,Balozi Dkt Batilda Salha Burian, ameonya watu wenye nia ya kusherehekea mwaka mpya kwa kuchoma moto matairi barabarani kutothubutu kufanya hivyo, kwa kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha uharibifu wa miundombinu hiyo.
Balozi Dkt Batilda ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo alianza kwa kuwashukuru na kuwapongeza watu wa Mkoa wa Tanga kwa ushirikiano walioweza kuuonesha kwa serikali kwa ngazi zote kuanzia,mkoa,wilaya hadi vijiji.
Katika mazungumzo yake Mkuu huyo wa Mkoa alisema," Nashukuru kwa ushirikiano uliooneshwa na wananchi dhidi ya serikali yao, wametoa ushirikiano kwa Viongozi wa wilaya,kata hadi vijijini, wamedumisha amani na kuleta Utulivu Mkoani huku wakiendelea kuchapa kazi".
Aidha Balozi Dkt Batilda hakusita kuzungumzia hali ya chakula akisema, mwaka huu unaelezwa kuwa na mvua chache na pia zisizotabirika, ambapo hata hivyo mkoa utaendelea kuweka mikakati na kuwa karibu na wananchi katika kuhakikisha kunakuwa na mavuno ya kutosha kama ya mwaka jana.
Akizungumzia sherehe za kukaribisha mwaka mpya, Balozi Dkt Batilda alisema, imekuwa ikifanyika hivyo kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa watu kuumaliza mwaka salama na kuingia katika mwaka mwingine.
Kutokana na hali hiyo Balozi Dkt Batilda alisema, uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na ule wa Jiji la Tanga umeandaa kusanyiko maalum katika viwanja vya Uhuru Park kwa lengo la kuwakutanisha wananchi kusherehekea pamoja.
Amesema kuwa, katika viwanja hivyo vya Uhuru Park kutakuwa na sanaa mbalimbali, yakiwemo mapishi ya utamaduni wa Tanga akitolea mfano upishi wa maamri, maandazi,samaki wa kuchoma ambapo wananchi watakula chakula hicho wakiburudika kusherehekea mwaka mpya.
Licha hayo, amesisitiza wananchi hasa wakazi wa Jiji la Tanga, kushiriki shughuli hiyo kwenye viwanja vya Uhuru Park, eneo ambalo ulinzi utaimarishiwa vya kutosha ili wananchi kusherehekea maadhimisho ya mwaka mpya kwa hali ya usalama na amani.
Ameongeza kusema kuwa ,katika viwanja hivyo vya Uhuru Park,kutakuwa na Dua kabla ya fataki kupigwa na wataalam mahususi na kwa utaratibu maalum kwa lengo la kuukaribisha mwaka mpya, hivyo ni vyema wananchi wakaungana ili kusherehekea.





.jpg)




No comments