Breaking News

TAMUFO YAWAPONGEZA VIONGOZI WALIOTUNUKIWA TUZO YA BALOZI WA AMANI DUNIANI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) na Balozi wa Amani Stella Joel,akizungumza wakati wa hafla ya kutunuku Tuzo ya Ubalozi wa Amani Duniani kwa Viongozi mbalimbali.

......................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

UMOJA wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), kupitia viongozi wa umoja huo wamewapongeza mabalozi wote waliotunukiwa  hadhi ya  Balozi wa Amani Duniani (AMB) "Peace Ambassador (AMB)" na Greenling Peace Foundation.

Tuzo hizo zilitolewa na Mwenyekiti Mwanzilishi wa Greeling Global Peace Organization Zambia Prof Bishop Kennedy Songwe pamoja na mgeni rasmi wa hafla ya utoaji wa tuzo hiyo Balozi Prof. Askofu Rejoice Ndalima.

Katika hafla ya kutunuku tuzo hizo iliyofanyika Ukumbi wa Rungwe Hotel Jijini Dar es Salaam, ilihudhuriwa na wageni waalikwa, wawakilishi wa taasisi mbalimbli, wanaharakati wa amani na viongozi wa kimataifa.

Viongozi wa TAMUFO ambao ni Mabalozi wa Amani walitumia nafasi hiyo kuwapongeza wadau na Viongozi hao ambao ni mabalozi wa Amani kwa kutunukiwa hadhi hiyo jambo ambalo ni la kujivunia.

Akizungumza katika Kongamano na hafla hiyo Balozi wa Amani Stella Joel  ambaye ni Katibu Mkuu wa TAMUFO alihimiza Watanzania kuendelea kuilinda amani ya nchi yetu kwa nguvu zetu zote.

Alisema Upendo ni Amri iliyo kuu tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kila Mtanzania anapaswa kuwa na upendo kwani matunda ya Upendo ni Amani Uvumilivu, Utu Wema na mambo yote yaliyo ya haki.

“Tuitafute haki pasipo kushindana jambo litakaloifanya nchi yetu iendelee kustawi kwa kudumisha upendo, amani na mshikamano wa kitaifa,” alisema Joel.

Kwa upande wake Balozi wa Amani Dkt. Frank Richard ambaye ni Mlezi wa TAMOFO alisema katika kongano hilo watu 11 walitunukiwa Tuzo za  Ubalozi wa Amani wakiwemo  Viongozi wa Dini baada ya kutambuliwa kutokana kuhamasisha kudumisha amani bila ya kuchoka.

Naye Mkurugenzi wa Makumbusho ya Viumbe Hai Iliyopo jijini  Arusha Dkt. Christina Ngereza amewahimiza Watanzania kuendelea kudumisha utamaduni wetu tuliodumu nao kwa muda mrefu wa kuitunza amani yetu badala ya kujiingiza kwenye mambo ya kigeni  hasa kwa kundi la vijana.

“ Tutunze heshima na miiko tuliofundishwa na wazee wetu   ambayo ni kupendana kuheshimiana na hivyo kudumisha Amani na Utulivu katika nchi yetu,” alisema Dkt. Ngereza.  

Baadhi ya viongozi waliotunukiwa tuzo hiyo ni Balozi Dkt. Jacob Mutashi, Balozi Dkt. Gideon Lukindo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania  (TANAPA),  Balozi Dkt. Noelia Ansgary Myonga na Mrakibu wa Polisi (SP), Dkt. Ezekiel Kyogo.

TAMUFO ni mdau na mshirika wa makundi mbalimbali yanayohamasisha kudumisha amani nchini. 

Picha ya pamoja na viongozi waliotunukiwa Tuzo.
Picha ya pamoja.

 Brass Bend ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), iliyokuwa ikitoa burudani wakati wa utoaji wa Tuzo hizo.

No comments