NAIBU WAZIRI NDEGE AIPONGEZA SMAUJATA KANDA YA KASKAZINI
....................................
Na Mwandishi Wetu, Manyara
Naibu Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara (CCM), Regina Ndege
ameipongeza Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), Kanda
ya Kaskazini chini ya Katibu wake Ezekiel Tlanka kwa jitihada kubwa
wanayoifanya ya kuibua matukio ya ukatili na kuyatafutia ufumbuzi kwa
kushirikiana na taasisi zingine likiwemo Jeshi la Polisi.
Mhe. Ndege alitoa pongezi hizo Januari 11, 2026 katika hafla
fupi ya kukabidhiwa hati ya shukrani iliyotolewa na Smaujata kanda hiyo
kutokana na mchango wake uliofanikisha kikao cha Jumuiya hiyo kilichofanyika Desemba
23, 2025.
“Nimekuwa nikifuatilia utendaji wenu wa kazi na jinsi Smaujata
inavyoibua matukio ya vitendo vya
ukatili na kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na vyombo vingine likiwemo jeshi
letu la Polisi kupitia dawati la jinsia hakika mnafanya kazi kubwa sana ya
kuisaidia Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Ndege.
Ndege alitumia nafasi hiyo kuipongeza Smaujata Kanda ya
Kaskazini na viongozi wao wote chini ya katibu wake Ezekiel Tlanka na kueleza
kuwa kazi wanayoifanya ni ya kujitolea hivyo pindi atakapopata nafasi
ataendelea kuwapa msaada.
Aidha, Ndege alisema ataendelea kushirikiana na Smaujata kwa
karibu zaidi na kuhakikisha jamii inakuwa salama kwa kuzingatia Mkoa wa Manyara
ni miongoni mwa mikoa yenye changamoto ya kuwa na matukio mengi ya ukatili
hivyo unahitajika ushirikiano ili kukabiliana na vitendo hivyo na kuhakikisha vinakwisha.
Kwa upande wake Katibu wa Smaujata Kanda ya Kaskazini,
Ezekiel Tlanka, alisema mchango wa mbunge huyo unaonesha dhamira ya dhati na
vitendo ya kuunga mkono jitihada za Jumuiya hiyo katika mapambano ya vitendo
vya ukatili na unyanyasaji hasa katika kanda hiyo.
Tlanka aliomba viongozi wengine kuiga mfano wa kiongozi huyo kwa kujitoa kusaidia jumuiya hiyo ambayo imejikita kupambana na matukio hayo ya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.
Chanzo Smaujata Mkoa wa Manyara.





.jpg)




No comments