Breaking News

MADINI YATAJWA KUWA CHACHU YA UTAJIRI: CHENGULA ATOA ‘PASSWORD’ YA KUINGIA SEKTA HIYO

Katibu wa Kamati ya Uhusiano na Uenezi wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Mess Chengula  akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Amani na Upendo Duniani yaliyofanyika kitaifa Mkoa wa Shinyanga Februari 28, 2026, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wanaharakati wa masuala ya amani.

............................

Na Dotto Mwaibale, Shinyanga

KATIBU wa Kamati ya Mahusiano wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania na Balozi wa Amani Duniani, Mess Chengula, amewahimiza Watanzania kujitokeza kuwekeza katika sekta ya madini, akisema ni moja ya njia halali na zenye matokeo makubwa ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Chengula alitoa kauli hiyo Februari 28, 2026 mkoani Shinyanga wakati wa maadhimisho ya Siku ya Amani na Upendo Duniani yaliyofanyika kitaifa, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wanaharakati wa masuala ya amani.

Alisema kwa sasa Serikali imeielekeza nguvu kubwa katika kuimarisha sekta ya madini, jambo linalofungua milango kwa wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa kunufaika na rasilimali hiyo.

“Huu ni wakati sahihi kwa Watanzania kuingia kwenye sekta ya madini. Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira rafiki na fursa ni nyingi,” alisema Chengula.

Akieleza uzoefu wake binafsi, Chengula alisema aliingia kwenye sekta ya madini mwaka 2020 na tangu hapo ameweza kujifunza na kunufaika kwa kiasi kikubwa.

“Mwaka jana nilipoenda kutunukiwa kuwa Balozi wa Amani Duniani nilikwenda nikiendesha gari langu aina ya Harrier, lakini leo nimekuja kushuhudia wanaotunukiwa tuzo hizi nikiwa na V8 za kutosha,” alisema, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wa kimkakati katika madini.

Alifafanua kuwa watu wengi hufikiri utajiri katika madini unatokana moja kwa moja na kuchimba, lakini siri kubwa ipo kwenye umiliki wa vitalu.

Kwa mujibu wa Chengula Gharama ya kitalu kimoja ni takribani Sh. 50,000 ambacho leseni yake hugharimu takribani Sh. milioni 1.

Alisema mmiliki wa kitalu anaweza kuingia ubia na wachimbaji au wawekezaji wakubwa na kwamba endapo madini yatapatikana kwa wingi, thamani ya kitalu hupanda maradufu au zaidi.

Alisema wapo Watanzania wengi waliowekeza kimya kimya kwenye vitalu na sasa ni mabilionea kupitia ama kuuza vitalu vyenye madini au kuingia mikataba ya ubia yenye faida kubwa.

“Mtu mwenye nia ya kuwekeza asikimbilie kuchimba. Anza na kitalu. Hapo ndipo ‘password’ ya utajiri ilipo,” alisisitiza.

Katibu wa Kamati ya Uhusiano na Uenezi wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Mess Chengula akipongezwa na Profesa Bishop Stephano Nzowa wa African Graduate University kwa hutuba yake fupi aliyoitoa katika maadhimisho hayo.
Maadhimisho hayo ya siku ya Amani na Upendo yakiendelea

 Viongozi mbalimbali wapigania Amani nchini wakiwa katika picha ya pamoja kwenye maadhimisho.  hayo. Wanne kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Dkt, Alexius Revocatus Kagunze, ambaye alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari (Honoris Causa) katika Ustawi wa Jamii na Uongozi wa Biashara kutoka Christian Ministerial Training University (CMTU) cha nchini Zambia pamoja na kuteuliwa kuwa Balozi wa Amani Duniani (Peace Ambassador – AMB) na Greenling Peace Foundation kwa kutambua mchango wake katika kuhimiza amani, mshikamano na maendeleo ya kijamii.

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibaale namba ya simu 0754362990. 

.

No comments