MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI MKUTANO WA UTAWALA BORA USWISI

Na Mwandishi Wetu, Uswisi
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika kudhibiti rushwa unahitajika uongozi
imara pamoja na kuishirikisha jamii na wadau kuanzia ngazi ya watoto shuleni.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akishiriki
mjadala wa ngazi ya juu uliyohusu masuala ya Utawala Bora na kukabiliana na
Rushwa uliyofanyika katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF)
unaofanyika Davos nchini Uswisi.
Amesema rushwa imekua changamoto kubwa inayoleta
madhara zikiwemo rushwa za ndani ya mataifa na zile za kimataifa.
Akitoa uzoefu wa Tanzania katika kupambana na
rushwa, Makamu wa Rais amesema serikali imeweza kuendelea kufanikiwa kupunguza
kiwango cha rushwa kwa kuimarisha taasisi za utawala kama vile ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kuhakikisha anawezeshwa kwa rasilimali
fedha na rasilimaji watu, vifaa na uwezo wa kutumia teknolojia ili aweze
kufutilia matumizi ya serikali.
Pia Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea
kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kuwepo kwa mfumo wa
uangalizi kutoka Bunge la Tanzania kupitia kamati za bunge kama vile Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambazo hufanya ufuatiliaji wa matumizi ya serikali.
Makamu wa Rais amesema kwa kuzingatia serikali
hufanya manunuzi kwa asilimia kubwa, hivyo imeimarisha Mamlaka ya Usimamizi wa
Manunuzi ya Umma ili kudhibiti rushwa katika michakato ya manunuzi.
Pia amesema nchini Tanzania wadau mbalimbali na
watu binafsi hufanya ufuatiliaji wa matumizi ya serikali na mwenendo wa rushwa
kwa kutumia taasisi binafsi.
Halikadhalika amesema ripoti mbalimbali kutoka
kwa mashirika binafsi husaidia katika kutambua mwenendo wa vitendo vya rushwa
na hivyo kuweka mikakati ya kukabiliana navyo.
Makamu wa Rais amesema kuongezeka kwa matumizi ya
teknolojia pamoja na uwazi katika michakato mbalimbali ya uwekezaji hususani
katika sekta ya madini kumesaidia katika kupunguza vitendo vya rushwa.
Makamu wa Rais yupo nchini Uswisi ambapo anamwakilisha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani.
No comments