WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA UGANDA
...............................
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa Majaliwa amewasili
leo Januari 18, 2024 nchini Uganda akimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi na Serikali zisizofungamana
na Upande wowote (NAM) ulioanza tarehe 15 - 20 Januari, 2024.
Pia, Mheshimiwa atamwakilisha Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia katika mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la
G77+China utakaofanyika tarehe 21-22 Januari, 2024, Kampala – Uganda.
Ujumbe wa Waziri Mkuu katika Mikutano hiyo
utajumuisha viongozi waandamizi wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa January Makamba.
Mkutano wa NAM hufanyika kila baada ya miaka
mitatu na Mkutano wa mwisho, wa 18 ulifanyika jijini Baku nchini Azerbaljan
mwezi Oktoba, 2019. NAM ni umoja wa nchi na Serikali 120 zenye msimamo wa sera
ya kutofungamana na upande wowote.
Umoja huo ulianzishwa wakati wa enzi za vita
baridi ili kusaidia nchi wanachama wake kutoka mabara ya Asia, Afrika na Latin
Amerika kuondokana na ukoloni ili kuweza kujitawala kisiasa, kiuchumi na
kijamii.
Akiwa nchini Uganda Waziri Mkuu anatarajiwa
kushiriki kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Kundi la G77
na China kuanzia tarehe 21-22 Januari, 2024. Mkutano huo unaotarajiwa
kushirikisha nchi wanachama wapatao 134.
Kwa upande wake,Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikino wa Kimataifa Januari Makamba amesema kuwa katika mkutano huo
kutakuwa na ajenda muhimu zitakazojadiliwa na kuamuliwa na Wakuu wa nchi.
“Katika mkutano NAM kutakuwa na maazimio mahususi
yanayohusu masuala ya maendeleo ya uchumi, kijamii, ajira, ushirikiano wa
kikanda na kimataifa, amani na usalama na masuala mengine yanayohusu nchi hizi
zisizofungamana na upande wowote.”
Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano
kwenye masuala ya biashara, uwekezaji, kutokomeza umaskini, mabadiliko ya
tabianchi, amani na usalama katika mipaka, sekta ya afya, mandeleo endelevu, na
uchumi wa kidijiti.
Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni
ndiye mwenyekiti wa mkutano huo na anatarajiwa kukabidhiwa rasmi Uenyekiti wa
Kundi hilo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Cuba Mheshimiwa Miguel Mario
Diaz-Canel Bermúdez.






.jpg)




No comments