WANAHABARI SINGIDA WAJENGEWA UWEZO UELEWA MRADI WA EACOP
Afisa Mawasiliano wa Nje EACOP, Abbas Abraham, akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Singida wakati wa semina ya siku moja ya kuwajengea uelewa wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) iliyofanyika Juni 10, 2024 mjini Singida.
..............................................
Na Dotto Mwaibale, Singidani Blog
WAANDISHI wa Habari Mkoa wa Singida wamejengewa uelewa wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ili nao
wakawaeleweshe wananchi kuhusu faida ya mradi huo ambao ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
Afisa Mawasiliano wa Nje wa EACOP, Abbas Abraham akizungumza na waandishi
hao katika semina ya siku alisema mradi huo unaanzia Kabaale – Hoima nchini
Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania.
Alisema mradi huo una urefu wa jumla ya kilomita 1443 kati ya hizo kilomita
296 zipo nchini Uganda na kilomita 1147 zipo Tanzania. Bomba linapita katika
mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora,
Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Bomba vilevile linapita katika wilaya 24,
kata 134 na vijiji zaidi ya 180.
Alisema matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni za kimataifa za utafutaji
na uchimbaji wa mafuta na gesi za TOTAL, TULLOW na CNOOC ulibaini uwepo wa
mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5.
Abraham alisema kutokana na ugunduzi huo ilibainika uwezekano wa kuvuna
mapipa kati ya bilioni 1.2 hadi 1.7 na kuwa kufuatia mahusiano ya ushirikiano
ya muda mrefu na faida za kupitisha bomba nchini Tanzania Serikali ya Uganda na
wawekezaji wa mkondo wa juu waliamua kujenga mradi huo kupitia Tanzania kutoka
Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Akizungumzia lengo la mradi huo alisema ni kuwezesha mafuta
yatakayozalishwa nchini Uganda kusambazwa katika soko la ndani na sehemu
inayobaki kuuzwa nje kwenye soko la kimataifa kupitia bomba la mafuta.
Alisema bomba hilo la mafuta linapitia katika mikoa nane na wilaya ya 24
zaTanzania Bara ambayo ni .Kagera (Bukoba Vijijini, Muleba na Biharamulo), .Geita
(Chato, Geita, Bukombe na Mbogwe), .Shinyanga (Kahama Mjini), Tabora (Nzega
Vijijini, Nzega Mjini na Igunga), Singida (Iramba, Mkalama na Singida Mjini),
.Dodoma (Kondoa na Chemba), Manyara (Hanang na Kiteto) na Tanga (Kilindi,
Handeni Mji, Handeni Vijijini, Korogwe, Muheza na Tanga Mji).
Abraham alisema fursa zitakazopatikana katika mradi huo ni fursa mbalimbali
za kiuchumi na kibiashara katika hatua za awali za ujenzi mradi umetoa fursa
kwa watanzania kupitia makampuni ya watoa huduma kujiandikisha katika kanzi
data ya EWURA ambaye ni mdhibiti wa mkondo wa chini na kati katika sekta ya
uziduaji na vilevile kwa watanzania kujiandikisha kupitia kanzidata ya
nguvukazi iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye
Ulemavu kupitia kitengo cha TaESA.
Alisema hadi sasa mkataba wa awali wa makubaliano kati ya nchi ya Uganda na
Tanzania umesainiwa ambapo umepelekea kuingia majadiliano kati ya mwekezaji
(EACOP) na nchi husika na kuwa hatua za awali zimeendela kufanyika ikiwa ni pamoja na
tafiti mbalimbali mfano tafiti za kihandisi na kuwa majadiliano yalikwisha
fanyika katika masuala mbalimbali kama vile ajira, manunuzi na kazi za awali za
ujenzi, nautoaji wa mikataba kwa makampuni ya ujenzi.
Akizungumzia kuhusu ardhi ya mradi alisema imetengwa katika maeneo makuu
matatu ambayo ni maeneo ya kipaumbele, eneo la bomba (mkuza) na sehemu ya
matenki ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.
“Mradi huu una fursa nyingi za kiuchumi na kijamii na unatarajia kuleta
mabadiliko makubwa na manufaa kwa nchi zote mbili pamoja na wawekezaji na unatarajia
kuzalisha ajira na kuwezesha jumla ya wananchi watakaonufaika na fursa zaidi ya
10,000 wakati wa ujenzi ukilinganisha na wakati wa shughuli za awali kabla ya
ujenzi na wakati wa uendeshaji,” alisema Abraham.
Alisema mradi huo utawezesha pia kutoa fursa mbalimbali za biashara
zitakazotokana na mradi huo.
Alisema maeneo ya kipaumbele yatazingatia kambi za wafanyakazi (12),
hifadhi za mabomba na kiwanda cha kuweka plastiki (1) eneo la mkuza litakuwa
ni eneo litakapolazwa bomba pamoja na miundombinu mingine kama vituo vya
kuongeza msukumo (4), kupunguza msukumo (2), vituo vya umeme n.k; sehemu ya
kuhifadhi na kusafirisha mafuta – patakapojengwa matenki na jeti ya kupakia
mafuta kwenye meli.
Akizungumzia gharama za kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa bomba hilo alisema zinatarajia
kufikia takribani Sh. Trilioni 8 za Kitanzania na kuwa bomba hilo litajengwa na
kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya China na TULLOW ya
Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Alisema ushirikishwaji wa wananchi ni mkubwa kwani mradi huo umetoa ajira 200
kwa watanzania katika kazi za awali na vilevile kampuni 100 za kitanzania
zimepata kazi na watanzania wame elimishwa kuhusu mradi huo na manufaa yake
huku wafanyabiashara zaidi 2000 wamepitishwa kwenye fursa zilizopo kwenye
mradi.
Aidha Abraham alisema wakati mchakato wa kuanza kwa mradi huo ulizingatia
maombi ya wananchi ya sehemu husika za kupita kwa mradi huo akitolea mfano wa
jamii ya Kabila la Watatoga (WATATURU) wanaoishi kati ya Tabora na Singida ambao waliomba usipite kwenye makaburi
ya wapendwa wao waliotangulia mbele za haki kwani kwao kuyahamisha makaburi
hayo na kupoteza mabaki ya sehemu za miili yao hata kipande kidogo cha mfupa wa marehemu kwa jamii hiyo ina kuwa ni laana kubwa.
Abraham alitaja maeneo mengine waliyozingatia maombi ya wahusika waliopisha mradi huo ni yale yenye miti mikubwa yanayotumika kwa ajili ya
kufanyia matambiko na shughuli za kimila
Alisema jambo lingine lililofanyika kwa wananchi waliopisha ujenzi wa mradi
huo waliwalipa fidia huku wengine wakijengewa nyumba bora za kisasa katika
maeneo mengine hatua ambayo imewawezesha kujengewa nyumba hizo bora na kutoka
kwenye nyumba zao za awali za tembe walizokuwa wakiishi.
Abraham kupitia semina hiyo amewaomba wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanyika wakati wa utekelezaji wa mradi huo kwa kulinda miundombinu kwenye maeneo ambayo mradi huo unapita.
Wanahabari walioshiriki semina hiyo wameomba EACOP kuwashirikisha hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo hadi utakapo kamilika ili waweze kuwahabarisha wananchi na wadau wengine.
Kwa upande wake Mratibu wa Uhusiano wa Jamii EACOP, Josephat Kanyunyu alisema uhamishaji wa wanananchi kupisha mradi huo ulifuata sheria za nchi na kwa Mkoa wa Singida nyumba 31 za kisasa zimejengwa kwa wananchi waliotoa maeneo yao kupisha mradi huo huku wengine wakilipwa fidia.
Kanyunyu alisema kati ya nyumba hizo nyumba 19 zimejengwa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Nyumba 10, Iramba na Nyumba mbili Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.Afisa Mawasiliano wa Nje EACOP, Abbas Abraham, akisisitiza jambo kwenye semina hiyo.
No comments