BALOZI SHELUKINDO AFUNGUA JPC YA KWANZA KATI YA TANZANIA NA COMORO
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amefungua Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya
Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Muungano wa Visiwa vya Comoro katika
Ngazi ya Wataalam unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22-24 Julai
2024.
Akizungumza katika mkutano huo wa kihistoria, Balozi Shelukindo ameelezea
kuridhishwa kwake na ukuaji wa mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Visiwa
vya Comoro ambao umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitatu
iliyopita.
“Mzunguko wa biashara kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro umeongezeka kwa
kiasi kikubwa katika miaka mitatu iliyopita kutoka Dola za Marekani milioni
6.75 mwaka 2021 hadi Dola milioni 54.67 mwaka 2023”,alisema Balozi Shelukindo.
Balozi Shelukindo amesema ukuaji huo wa biashara ni mafanikio makubwa na
kusisitiza kuwa bado kuna haja kwa nchi hizo mbili kuongeza uwigo wa
ushirikiano wa kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo kwa tija ya pande zote
mbili.
Amesema mikutano hiyo ya Tume ya Pamoja ya Ushirikiano inatoa fursa kwa
nchi hizo mbili kupanua na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kupitia nyanja
mbalimbali.
Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina nia ya dhati ya kupanua
ushirikiano na Visiwa vya Comoro kupitia sekta mbalimbali, zikiwemo diplomasia,
ulinzi na usalama, masuala ya kisheria, fedha, biashara, uwekezaji, utalii,
kilimo, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, miundombinu, TEHAMA, afya, elimu,
michezo, sanaa na utamaduni.
Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa Visiwa vya Comoro Mhe. Balozi Fatima
Alfeine akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo ameeleza kuwa mkutano huo
hautalenga kujadili namna ya kutatua changamo pekee bali kwa pamoja kuibua
maneo mapya ya ushirikiano yatakayo chochea zaidi maendeleo ya kiuchumi na
kijamii kwa pande zote mbili.
“Kutokana na uhimu wa mkutano huu wa kihistoria, ujumbe wetu umejumuisha
wataalam kutoka sekta zote muhimu, kwa sababu tuna dhamira ya dhati sio tu ya
kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na undugu wa kihistoria uliopo kati yetu
bali kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunaweka mazingira wezeshi na rafiki zaidi kwa
wananchi wa pande zote mbili kunufaika zaidi kiuchumi kupitia fursa lukuki
zilizopo”. Ameeleza Balozi Fatima Alfeine.
Mkutano huo wa siku tatu unashirikisha wadau kutoka Sekta za Diplomasia,
Sheria, Ulinzi, Biashara, Kilimo, Biashara, Uwekezaji, Uchumi wa Buluu, ICT na
Nishati.
No comments