RAIS SAMIA: SERIKALI ITAENDELEA KUKABILI UPUNGUFU WA MADAKTARI NCHINI
Na Sophia Kingimali.
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kukabiliana na
upungufu wa Madaktari kwani kadri nchi inavyopiga hatua kwenye maendeleo ndivyo
uhitaji wa watumishi katika sekta ya afya unavyozidi kuongezeka.
Hayo amesema leo Julai 31,2024 katika kilele cha kongamano ya kumbukizi ya
tatu ya Rais Mstaafu wa awamu ya tatu hayati Benjamini Mkapa ambapo kongamano
hilo liliandaliwa na Taasisi ya Benjamini Mkapa(BMF).
Amesema Serikali inafahamu umuhimu wa sekta hiyo na inatambua upungufu
uliopo hivyo ametoa rai kwa wizara zote ambazo zinahusika na uajili pindi
wanapotoa ajira katika sekta waajiri na madaktari wa mkataba ili waweze
kujitolea katika hospitali na vituo vya afya vilivyopo nchini.
“Hapa nataka niwe shahidi wa upungufu uliopo kwani ninapozunguka mikoani na
wilayani changamoto namba moja ninayokutana nayo ni upungufu wa watumishi
katika sekta ya afya na elimu na hii ni kwa sababu ya ongezeko la watu na
tunaendelea kuzaliana kila siku kwa hiyo mahitaji ni makubwa na ndio maana kila
tunavyoajiri watumishi bado wanakuwa hawatoshi”,Amesema Dkt Samia.
Aidha amesema ajira hizo zinaendana na ukuaji wa uchumi ndio maana
inapopatikana nafasi ndogo uchumi ukiongezeka na watumishi sekta ya afya na
elimu kunakuwa na upungufu.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema miongoni mwa mambo
yaliyoibuka kwenye kongamano hilo ni uzalishaji wa
madaktari,Wauguzi,wafamasia,wataalamu wa maabara lakini kukosekana kwa ajira
kwa wataalam waliopo.
Amesema hivyo miongoni mwa maazimio ni pamoja na kuhakikisha hospitali
zinaajili watumishi wa mikataba ambapo mchakato wa bima ya afya kwa wote
utakapokamilika utaziwezesha hospitali nchini kuajiri watumishi wa mikataba.
“Madaktari na wataalam tunazalisha wengi kupitia vyuo vyetu nchini na
hatuwapi ajira lazima tuangalie namna ya kutatua changamoto hii”,Amesema.
Ameongeza kuwa watakaa na mabaraza ya wanataaluma wakiwemo
MAT,wafamasia,wauguzi,maabara ili wakubaliane namna bora ya kudhibiti watumishi
wa afya ambao wapo barabarani.
Nae,Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo(BMF)Dkt Hellen Senkoro amesema katika
kipindi cha miaka 18 tangu kuanza kwa taasisi hiyo imeweza kutoa jumla ya ajira
13,000 katika sekta ya afya ambapo zinajumuisha wataalam 7000 wanaojulikana
kama Mkapa Fellows na wahudumu ya afya ngazi ngazi ya jamii 6,000.
Ameongeza kuwa pia Taasisi hiyo imetoa ufadhiri wa masomo kwa wanafunzi
1,150 ambao walikwenda vyuoni na kuhitimu katika fani mbalimbali za afya na
wengine wanaojiendeleza wakiwa kazini.
No comments