MRADI WA SLR WATENGA EKARI 28,000 UREJESHAJI UOTO WA ASILI
Hayo yamebainishwa Julai 31, 2024 Mkoani Iringa na Mratibu wa Kitaifa wa
Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati wa mahojiano na waandishi wa vyombo vya
habari katika kikao cha siku moja cha kamati ya kitaifa ya usimamizi wa mradi
kilichopokea taarifa ya mradi huo.
Dkt. Mapunda amesema tangu kuanza kwa mradi mwaka 2021, wataalamu
walibainisha baadhi ya maeneo yaliyopo ndani ya halmashauri zinazotekeleza
mradi ili kuonesha juhudi na hatua mahsusi zinazochukuliwa na Serikali kwa
kushirikiana na wadau katika urejeshaji wa uoto wa asili.
“Moja ya eneo ambalo tunaweza kujivunia kwa sasa katika mradi ni urejeshaji
wa uoto wa asili…kati ya vijiji 54 vya mradi tuna vijiji ambavyo kwa sasa suala
la uoto wa asili limeleta manufaa manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi”
amesema Dkt. Mapunda.
Ameongeza kuwa kupitia mpango wa urejeshaji, baadhi ya maeneo yaliyopewa
kipaumbele ni pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji, huduma za mifumo ikolojia
pamoja na shughuli za kilimo mseto.
Aidha Dkt. Mapunda amesema kupitia uhifadhi misitu jamii, mradi umewezesha
shughuli endelevu na wezeshi ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji wa kisasa na
kusaidia uhifadhi wa mazingira na kufanya usimamizi wa rasilimali zilizopo na
kuandaa mpango matumizi bora ya ardhi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kuhakikisha Tanzania inafikia
malengo ya kidunia ya kurejesha ekari Milioni 2.5 za uoto wa asili nchini
ifikapo mwaka 2030.
Kuhusu vipaumbele vya bajeti ya mradi kwa mwaka 2024, Dkt. Mapunda amesema
jumla ya vipaumbele vitano vimeainishwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za mradi ambapo moja ya kipuambele hicho ni usimamizi wa biashara ya
kaboni.
Ametaja vipaumbele vingine ni kuwezesha wakulima kutekeleza shughuli za
miradi ya mabadiliko ya tabianchi, ufugaji endelevu, kuhamasisha shughuli
mbadala za kiuchumi pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya shughuli za
uzalishaji mali.
Kwa upande wake Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi
wa Mazingira (IUCN), Doyi Mazenzele amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na
Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuweka mikakati ya pamoja kwa kuendelea
kuhimiza jamii kutambua umuhimu wa utunzaji wa bioanuai ambazo zinachangia
upatikanaji wa huduma ikolojia.
“Tumeendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Wizara
mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kitaalamu wananchi na wasimamizi wa
miradi katika maeneo ya halmashaur” amesema Mazenzele.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bw. Robert
Masunya amesema Halmashauri hiyo imeendelea na juhudi mbalimbali za uhifadhi wa
mazingira na urejeshaji wa uoto wa asili kwa kuhimiza shughuli wezeshi
zisizoharibu mazingira ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Tumeendelea kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinapewa kipaumbele katika
maeneo yote ndani ya Halmashauri ambayo yanatekeleza mradi kwa ikiwemo ulinzi
wa vyanzo vya maji kwa kuhamasisha wananchi kutunza maeneo hayo" amesema
Masunya.
Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya
Makamu wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya
utekelezaji wa mradi huo.
Mradi huo ulioanza mwaka 2021 unatarajia kukamilika mwaka 2025 na kunufaisha
jumla ya Mikoa 5, Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54. Halmashauri
zinazonufaika na mradi ni Iringa Vijijini, Mbeya, Mbarali, Sumbawanga vijijini,
Tanganyika na Mpimbwe.
1. Katibu Tawala
Msaidizi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Bw. Salehe Msampa akizungumza jambo wakati wa kikao cha kamati ya kitafia ya
usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai
Tanzania (SLR) kilichofanyika Mkoani Iringa Julai 31, 2024.
1. Mwakilishi kutoka Wizara ya Maji, Bw. Modestus Herman akizungumza jambo wakati wa kikao cha kamati ya kitafia ya usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) kilichofanyika Mkoani Iringa Julai 31, 2024.
1. Wajumbe wa kikao cha kamati ya kitaifa ya usimamizi wa Mradi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika Mkoani Iringa Julai 31, 2024.
1. Mtaalamu Mshauri wa Mradi Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) akizungumza jambo wakati wa kikao cha kamati ya kitafia ya usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) kilichofanyika Mkoani Iringa Julai 31, 2024.
1. Wajumbe wa
kamati ya kitaifa ya usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na
Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa
kikao cha kamati ya kitafia ya usimamizi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa
Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) kilichofanyika Mkoani Iringa
Julai 31, 2024.
No comments