MABONDIA WA MAFIA BOXING PROMOTION WATEMBELEA YATIMA JIJINI TANGA
Na Mashaka Kibaya, Tanga
.............................
MABINGWA wa Masumbwi katika mapambano ya 'Knockout ya Mama' Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan, wamerejesha fadhila kwa jamii baada ya kuamua kugawana sehemu ya
walichokipata kufuatia ushindi mkubwa
kwenye mpambano wao wa ngumi ulifanyika hivi karibuni.
Mabondia hao kutoka Kampuni ya Mafia Boxing Promotion wametua Jijini Tanga
baada ya mapambano yao Jijini Dar es Salaam ambapo walitembelea Kituo cha
kulelea Watoto Yatima pia walikutana na mama lishe kwenye masoko.
Katika Kituo cha kulelea Watoto Yatima cha Green Cresent Foundation timu
hiyo ya mabondia na Uongozi wa Mafia Boxing Promotion waligawa vyakula,vinywaji
laini na majiko ya gesi, misaada ambayo iliibua faraja kwa walengwa na
wasaidizi wao.
Mbali na kutoa misaada hiyo kwa kundi hilo la Yatima lenye Makao yake Mitaa
ya Bombo Jijini Tanga, lakini pia mabondia hao walitembelea Masoko ya Makorora,
Mgandini na Mlango wa Chuma kote wakigawa Majiko ya Gesi kwa Mama lishe.
Lengo la ugawaji wa Majiko hayo ya Gesi ni ili kuleta mabadiliko chanya kwa
Wajasiriamali hao kuondokana na matumizi ya kuni na Mkaa na hivyo kupunguza
vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Katika mazungumzo yake kwenye ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu Matangazo na
Uzalishaji, Omari Clayton alisema,ushindi huo wa mabondia hao Vijana wa
Kitanzania kutoka Mafia Boxing Promotion ni matokeo ya hamasa kubwa kutoka kwa
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Clayton alisema ahadi ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Vijana iliamsha
ari,chachu na motisha kubwa ya ushindi kwa mabondia hadi kuweza kufanikiwa kunyakuwa mikanda yote
iliyoshindaniwa.
"Baada ya Mama (Rais) kuwaahidi Vijana nao wakapata ari ya kufanya
vizuri kama ilivyo kwenye mpira wa miguu...sasa kile walichokipata wakasema
hapana tuna wadogo zetu mayatima na hata mama lishe tukashiriki nao"
alisema Omari Clayton.
Kapteni wa mabondia hao Ibrahim Mustafa mshiriki na Mshindi wa WBC Afrika
alielezea faraja yake baada ya wao kufanikiwa kupeperusha vyema bendera ya
Tanzania ambapo alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake
kwenye medani hiyo ya mchezo wa ngumi.
Aidha bondia huyo alisema kwamba,katika mapambano ya 'Knockout ya Mama'
licha ya hamasa waliyoipata kutoka kwa Rais pia wanaamini kuwa Watanzania
wakiwemo Yatima na wapenzi wa michezo waliwaombea kwa Mungu na ndio sababu na
wao wakaona vyema kuungana nao.
Bi. Zainati Saidi ni Mama Mlezi wa Kituo cha Yatima cha Green Cresent
Foundation, amewashukuru Mafia Boxing Promotion kwa misaada waliyowapatia huku
akiungana na watoto Yatima waliokuwepo kuwaombea Mungu mabondia kuendelea
kufanya vizuri.
Vilevile kwa upande wa Mama lishe waliopatiwa majiko ya Gesi waliwasilisha Shukrani zao kwa mabondia wa Mafia Boxing Promotion na Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia vitendea kazi hivyo wakiamini kuwa vitawasaidia katika kuimarisha utendaji kazi wao.
Msaada ukitolewa.
No comments