MBUNGE FYANDOMO AWAHAMASISHA WAKAZI DAR KUJIANDIKISHA DAFTARI LA MPIGA KURA
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo ambaye alikuwa mgeni rasmi akihutubia kwenye mahafali ya 11 ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi na mahafali ya 14 kwa wahitimu wa elimu ya awali katika Shule ya ABC Capital iliyopo Mongo la Ndege Ukonga jijini Dar es Salaam.
......................
Na Kulwa Mwaibale, Dar es Salaam
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo amewahasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam hususan wa Kata ya Ukonga kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwishoni mwa Novemba mwaka huu.
Fyandomo alitoa hamasa hiyo mwishoni mwa juma lililopita kwenye mahafali ya 11 ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi na mahafali ya 14 Kwa wahitimu wa elimu ya awali katika Shule ya ABC Capital iliyopo Mongo la Ndege, Kata ya Ukonga.
Sambamba na kuwahasa kugombea nafasi za uongozi, Mbunge huyo aliyekuwa mgeni rasmi amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Mpigakura la Serikali za Mitaa ili waweze kuchagua na wao kuchaguliwa kwa sababu ni haki yao kikatiba.
"Ndugu zangu nawaomba kwa dhati, nendeni mkajiandikishe ili muweze kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kabla zoezi hilo alijafika tamati," alisema Fyandomo.
Aliongeza kuwa kila mwenye sifa ya kupiga kura ajitokeze kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi huo kwani ni haki yake kikatiba kuchagua na kuchaguliwa.
"Bila kujali jinsi jitokezeni kugombea nafasi yoyote kwenye uchaguzi huo kwani ni haki yenu kikatiba.
Fyandomo aliwaomba wakati huo wa uchaguzi wawachague viongozi wa CCM ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan aliyelitanyia makubwa taifa letu tangu awe rais.
"Wakati wa kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa tuwachague kutoka CCM ili mumuunge mkono Rais Samia anayelifanyia makubwa taifa letu," alisema Fyandomo.
Aliongeza kuwa kwa muda mfupi ambao Mama Samia amekaa madarakani amefanya makubwa, amejenga miradi ya barabara, madaraja, umeme, ujenzi wa shule zilizojengwa hadi vijijini, miradi ya maji, afya, sekta ya uvuvi, usafirishaji wa anga, majini na nchi kavu ambapo amefanikiwa kukamilika kwa mradi wa treni ya umeme ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
" Nani asiyeona maendeleo aliyoyafanya mama yetu na nani anayeweza kufanya mambo makubwa kama aliyoyafanya Rais Samia?' alihoji mbunge huyo.
Fyandomo aliwaasa wakazi wa Dar es Salaam mwakani wakati wa Uchaguzi Mkuu kumchagua kwa kishindo Rais Samia ili aendelee kulifanyia makubwa taifa letu.
Akizungumza kwenye mahafali hayo aliwapongeza walimu, mkurugenzi, wazazi na wanafunzi wa Shule ya ABC. Capital kwa ushirikiano wao unaoifanya shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma, nidhamu na usafi na kuwa mfano miongoni mwa shule wilayani Ilala.
Aliwasihi wazazi wa watoto waliohitimu elimu ya darasa la saba na wanaondelea kusoma kwenye shule hiyo wawe mabalozi kwa wazazi wengine ili nao wawapeleke watoto wao kwenye shule hiyo inayowaandaa vizuri watoto katika kila nyanja.
"Wazazi wenzangu wenye watoto wanaosoma hapa ABC Capital mmeona jinsi vijana wenu walivyoiva kuanzia kitaaluma, nidhamu, usafi, mambo ya urembo, utamaduni wa asili yetu, mumewaona wataalamu wa sayansi, mainjinia mpaka wafaransa, nendeni mkawe mabalozi wazuri kwa wazazi wengine ili wawalete watoto hapa kama nitakavyofanya mimi," alisema mbunge huyo.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ezra Alfred akizungumza kwenye mahafali hayo alimshukuru Mbunge Fyandomo kukubali kuwa mgeni rasmi akawataka wazazi waendelee kushirikiana nao ili wazidi kuinua elimu kwa watoto wao.
"Mafanikio haya mnaoyaona kwa watoto wenu yametokana na ushirikiano wenu mzuri kwetu, nitoe rai muendelee kulipa ada kwa wakati na mtupe ushirikiano wa hali na mali tutafanya makubwa kwa watoto wenu na shule yetu itazidi kuongoza kwa ubora, " alisema mkuu huyo wa shule.
Meneja wa shule hiyo, Patricia Mwapunga akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi ambaye hakuhudhiria kwenye mahafali hayo aliwapongeza walimu kwa kuwafundisha vyema watoto ambao wapo vizuri kwa kila eneo.
"Wakati tulipoanza kuwafundisha watoto wa darasa la awali walikuwa hawawezi kuongea lakini kwa miaka minne waliyokaa hapa wanaweza kuongea vizuri, pongezi kwenu walimu," alisema meneja huyo.
Wanafunzi waliohitimu Darasa la Saba, wale waliohitimu elimu ya awali watakaoanza Darasa la Kwanza mwakani na wale wa madarasa mengine walionesha umahiri mkubwa kitaaluma, sanaa ya maigizo ambapo waliigiza wakifanya shughuli za kibunge, urembo, ngoma za asili ambapo waliofanya vizuri katika kila eneo walipewa zawadi.
Wanafunzi wa kike wanaoishi bweni walikabidhiwa kombe na mgeni rasmi kwa kuibuka kidedea kwa usafi.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ezra Alfred akizungumza kwenye mahafali hayo
Meneja wa shule hiyo, Patricia Mwapunga akizungumza
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo akimkabidhi mtoto wake
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo, akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo, akikabidhiwa zawadi mhitimu Glory Maswi kwa kuwa kinara kati ya wahimtu wote kwa kufanya vizuri katika maeneo mengi.

Wahitimu wakitoa burudani ya kwaya.
Wageni waalikwa na wazazi wakiwa kwenye mahafali hayo.
Burudani zikiendelea
No comments