NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS KHAMIS HAMZA KHAMIS ASEMA SERIKALI YASAINI MIRADI 63 YA BIASHARA YA KABONI
.............................
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imesajili miradi 63 ya biashara ya kaboni kupitia sekta mbalimbali.
Mhe. Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Novemba 06, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Amani Mhe. Abdul Yussuf Maalim aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuongeza wigo wa biashara ya kaboni ili kupunguza uharibifu wa ukataji wa misitu nchini.
Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis ametaja sekta
zilizo katika miradi iliyosajiliwa ni pamoja na Kilimo (asilimia , Nishati (asilimia
33), Misitu (asilimia51), Mifugo (asilimia 5) na Usimamizi wa taka (asilimia
3).
Amesema kati ya miradi iliyosajiliwa kupitia Sekta ya Misitu ni minne inahusisha shughuli za upandaji miti, miradi 20 ni kwa ajili ya kupunguza uharibifu na upotevu wa misitu na miradi mitano ni kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili.
Aidha, Mhe. Khamis ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) ambao unahamasisha matumizi ya nishati safi za kupikia ikiwemo gesi asilia, nishati jadidifu, mkaa mbadala na umeme ambazo zinaweza kuchangia katika Biashara ya Kaboni na kupunguza matumizi ya kuni na ukataji wa misitu.
Halikadhalika, amesema Serikali imeandaa na inatekeleza Sera ya
Taifa ya Uchumi wa Buluu 2024 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya
Uchumi wa Buluu (2024 – 2034).
“Mheshimiwa Mwenyekiti katika Sera hii ya Taifa ya Uchumi wa Buluu tumeweka mikakati ya kuhamasisha matumizi ya hati fungani za buluu na biashara ya kaboni katika shughuli za rasilimali za Uchumi wa Buluu kwa lengo la kuongeza wigo wa biashara ya kaboni nchini ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira,“ amesema.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali
inachukua mipango madhubuti kuhakikisha misitu inakuwa sehemu ya mapato kupitia
biashara ya kaboni katika vijiji, shehia na wilaya kwa kuwashirikisha wananchi
katika kuihifadhi.
No comments