Breaking News

WATURUKI ZANZIBAR WADAIWA KUTUMIA YATIMA KUJIPATIA MAMILIONI YA FEDHA

Watoto wakihudumiwa chakula na Taasisi ya  The Institute of Holistic Education of  Zanzibar  inayomiliki Sekondari ya Bweni ya Wavulana ya Olgun  iliyopo Mkoa wa Magharibi  “B”, Zanzibar.

...............................


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIA wa Kituruki wanaoendesha Taasisi ya  The Institute of Holistic Education of  Zanzibar  inayomiliki Sekondari ya Bweni ya Wavulana ya Olgun  iliyopo Mkoa wa Magharibi  “B”, Zanzibar wanadaiwa kuingia katika kashifa ya kujipatia mamilioni ya fedha kupitia yatima.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa waturuki hao wamekuwa wakiwapiga picha watoto hao wakiwa kwenye makazi duni na kuwatumia wafadhili hao ambao huwatumia fedha.

Mmoja wa aliyekuwa mfanyakazi wa taasisi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Salim Hamad Mbaruku akizungumza na waandishi wa habari alisema mambo yanayofanyika ndani ya taasisi hiyo ambayo pia inafundisha elimu ya dini kwa watoto wa madrasa ni kinyume kabisa na misingi ya dini hiyo.

Mbaruku alisema tangu ianzishwe taasisi hiyo imeweza kujenga shule hiyo kwa gharama kubwa kupitia ufadhili wa watu wa Uturuki ambao wanaamini wanasaidia yatima wa Zanzibar ambao wanatozwa ada kubwa wakati ilipaswa wasome bure.

Mbaruku alidai  viongozi wa taasisi hiyo wamekuwa wakisaidiwa na baadhi ya wanzanzibar ambao sio waaminifu kufanya vitendo hivyo ambapo wamefikia hatua ya kujenga vibanda vya nyasi katika eneo la taasisi hiyo  na kuwapiga picha watoto hao  mbele ya vibanda hivyo na kuzituma kwa wafadhili hao  na kuwafahamisha watoto hao yatima huishi kwenye vibanda hivyo.

Wafadhili hao baada ya kuziona picha hizo huwaonea huruma watoto ambao sio yatima na kutuma mamilioni ya fedha ili wajengewe makazi bora ya kuishi fedha zinazoishia mifukoni  mwa wajanja hao.

Mbali ya kujenga vibanda hivyo,  inadaiwa wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani viongozi wa taasisi hiyo huwatuma baadhi ya wafanyakazi wao kwenda kuwachukua watoto majumbani mwao kwa ajili ya kuwapa futari.

Inadaiwa  kuwa  katika kila sahani ya futari wanayopewa  huwekwa nanasi zima na kupigwa picha, baada ya zoezi hilo mananasi hayo huondolewa bila kuliwa.

Inadaiwa picha hizo zinatumwa Uturuki kwa wafadhili na kueleza taasisi hiyo imekuwa ikitoa mlo kamili kwa watoto hao.

Mbaruku anayedai kufanya kazi ya mwalimu wa madrasa kwenye taasisi hiyo kwa miaka mitano alisema alikuwa akilipwa Sh. 150,000 na kusainishwa kwa jina la mtu mwingine anayeitwa Salim Othman na hata alipohoji wahusika walikuwa hawampi majibu ya kueleweka zaidi ya kumueleza kuwa alikuwa akipewa fedha hizo kama sadaka tu na si vinginevyo.

“ Hali sio nzuri kwenye taasisi hiyo tunajiuliza hivi watanzania wanaweza kufanya mambo ya namna hii huko Uturuki na  mamlaka zinazohusika zipo kweli kwa sababu mambo haya yanafanyika hapa Zanzibar bila ya kificho tunaomba watu wa Ustawi wa Jamii, Wizara ya Elimu  wafuatilie haya mambo,” alisema Mbaruku kwa masikitiko.

Mbaruku alisema hata watu wa Idara ya Uhamiaji wanapaswa kufika kwenye taasisi hiyo kujua uhalali wa vibali vya kuishi na kazi ambazo wameziainisha waturuki hao.

Inadaiwa wafanyakazi wanapodai kupewa mikataba ya kazi huambiwa waende popote pale hata huko juu hawatapata msaada kwa sababu taasisi hiyo ina mtandandao mkubwa wa watu wa kuwasaidia serikalini na baadhi ya viongozi wakubwa wa dini.

Mbruku alisema licha ya kuwataka viongozi hao wampe haki yake baada ya kumuachisha kazi wamegoma na kusisitiza kuwa hakua mfanyakazi wao kwa kuwa hana mkataba.

Aliongeza kusema , katika hali ya kushangaza Novemba 5, 2024 alipofika kudai haki yake mmoja wa kiongozi wa taasisi hiyo alimkabidhi barua iliyoandikwa Septemba 28, 2024 ambayo mwandishi wa habari hii anayo nakala yake iliyoandikwa hivi:

“ Mheshimiwa Salum Mbarouk Othman, Taasisi yetu imekuwa ikitoa msaada wa kifedha kwa muda mrefu ili kusaidia shughuli zako za dini ya Kiislamu. Hata hivyo, kufuatia tathimini iliyofanywa, baraza la uongozi limeamua kusitisha msaada wa kifedha kwako kwa sababu ya kukosa kuzingatia kwa umakini mahitaji ya Kiislamu” ilisomeka barua hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Ibrahim.

Aidha, Mbaruku alisema sababu ya kuachishwa kazi imetokana na uongozi wa taasisi hiyo kumtaka aende akasimamie madrasa na msikiti uliopo eneo la Maungani  ambapo alitaka waandikiane mkataba kwa kazi hiyo mpya sambamba na nyumba aliyoahidiwa angekaa bure na familia yake.

“Nilimuambia boss Ibrahim kuwa kama ananihitaji kunihamishia Maungani baada ya kuridhishwa na kazi nzuri nilioifanya kwenye madrasa ya awali nahitaji anilipe shilingi laki nne ili ziniwezeshe kukidhi mahitaji ya familia yangu hivyo anipe mkataba ambao utaelezea nyumba nitakayo kaa nitaishi bure ili nisije nikasumbuliwa baadae,” alisema Mbaruku.

Mbaruku alisema baada ya kumuambia hivyo boss wake huyo alikasirika na kuchukua uamuzi wa kumuondoa kazini na hiyo ndio sababu ya kutokea kwa chokochoko zote hizo na sio kukiuka taratibu za dini ya kiislamu alizozitoa kwenye barua aliyokabidhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Abii Rashid Rashid alikiri kumfahamu Mbaruku ambapo alikana hakuwa mfanyakazi wa taasisi hiyo.

“Mbaruku sio mfanyakazi wetu kwa sababu hana mkataba kama anao awaonesheni hapa alikuwa anafanya kazi za kusaidia kufundisha madrasa sisi tulikuwa tunampa hela kama sadaka na kama anataka kuchafua taasisi yetu tutamshitaki yeye na vyombo vya habari kwa sababu taasisi yetu ni kubwa na ipo dunia nzima na tunawanasheria wetu,” alisema Rashid.

Watoto wakipata chakula na juu ni vibanda vinavyodaiwa kujengwa na taasisi hiyo ambavyo watoto hao hao upigwa picha na kuzituma kwa wafadhili wa kituruki wakielezwa ndivyo vinavyotumiwa kulala watoto hao wakati sio kweli.  

Watoto wakishiriki michezo katika taasisi hiyo.
Muonekano wa majengo ya shule yaliyojengwa na taasisi hiyo.

No comments