DEREVA NA KONDAKTA WAKE WADAKWA NA POLISI WAKISAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA
Na Mashaka Kibaya, Tanga
WATU wawili akiwemo Dereva Hashimu Juma Mohamed
(46) na Kondakta Ramadhani Ismail Mbaruku (28) wanashikiliwa na Polisi mkoani
Tanga wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya 'Mirungi' kwa kutumia gari lenye
namba za usajili T 689 EJJ aina ya Coaster Hino.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika taarifa yake aliyoitoa Jana kwa
Waandishi wa habari Ofisini kwake Jijini Tanga.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni matokeo ya msako
uliofanywa na Polisi Disemba 10 mwaka huu huko Kijiji cha Makuyuni tarafa ya
Mombo Wilayani Korogwe, watu hao walikamatwa wakitokea Mkoani Kilimanjaro
kuelekea katika jiji la Dar es Salaam.
ACP Mchunguzi alisema, katika upekuzi wa gari
watuhumiwa walikutwa na Mirungi bunda 962 sawa na Kg 411.05 dawa ambazo
zilikuwa zukisafirishwa kwa lengo la kuingizwa Sokoni.
Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani wakati wowote
baada ya taratibu za kisheria kukamilika huku Kamanda Mchunguzi akiweka bayana baadhi ya mafanikio waliyoyapata kwa kipindi cha
Nov hadi Disemba 2024.
Alisema,kwa upande wa kesi zilizofikishwa
Mahakamani mwezi Novemba hadi Disemba 2024 watuhumiwa wanne wamehukumiwa
vifungo vya maisha na wengine watatu wamehukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo
miaka 30.
Amemtaja Mwamini Mgeja (32) mkulima na mkazi wa
Kilindi Asilia kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto
wake wa kambo mwenye Umri wa miaka tisa (9) na Jonas Alphan (38) mkulima na
mkazi wa Gombero Kilindi aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la
kumbaka mtoto wa miaka 4.
Mwingine aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela ni
Rajabu Juma , mkulima na mkazi wa Mafleta Kilindi baada ya kupatikana na hatia
ya kumbaka mtoto wa miaka 17 huku Salimu Riziki na Athuman Salumu Jumaa
wakihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyany'anyi wa kutumia
silaha na miaka 20 jela kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha Sheria.
Pia Richard Kiwango Shelukindo (45) mkulima na
mkazi wa Kwaludege Handeni amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la
kulawiti mtoto wa miaka 5 na Mansuri Omari (19) mkulima na mkazi wa Kwakibuyu
Pangani amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka binti mwenye
Umri wa miaka 16.
Wito umetolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Tanga
kwa wananchi wote kuelekea msimu wa Sikukuu za mwisho wa mwaka Krismasi na
mwaka mpya ,Madereva kuzingatia Sheria za Usalama barabarani kuepuka mwendo
Kasi ,ulevi wakati wa kuendesha magari.
Aidha Kamanda Mchunguzi amewataka Wananchi wote kuzingatia kanuni,sheria na taratibu za kudumisha Amani na Usalama wa Mkoa wa Tanga.
No comments