WANACHUO TANGA MBARONI KWA KUHUSISHWA NA WIZI WA KIMTANDAO
............................
Na Mashaka Kibaya, Tanga
MWANAFUNZI wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Peter
Michael Babuya (24) na wenzake wengine watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi
Mkoani Tanga wakituhumiwa na makosa ya Wizi kwa njia ya Mtandao.
Wengine wanaoshikiliwa pamoja na Mwanafunzi huyo
ni Said Amiri 'Mofisamchayungu' (21) mkazi wa Kimara Dar es Salaam, Athumani
Amiri Athumani (24) mkazi wa Mbezi mwisho Dar es Salaam.
Pia wamo Brayani Matina Mayunga 'Festo Madenge'
(26) mkazi wa Mombasa Ukonga Dar es Salaam na Wakala James John Nathaniel (24)
mkazi wa Kitunda Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius
Mchunguzi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema, watuhumiwa hao
wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Alisema,Watuhumiwa hao wamekuwa wakijifanya mawakala
wa kujitegemea (Freelancers) wa Kampuni za Tigo, Vodacom na Airtel na kuiba
fedha kiasi cha Shilingi 20,390,000 (Milioni Ishirini na laki tatu na tisini
elfu) kwa njia ya Mtandao Mali ya Abdul Hemed Shedafa mfanyabiashara na mkazi
wa Muheza Mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi baada ya uchunguzi
wa kitaalamu kufanyika ndipo ilipobainika kuwa Watuhumiwa walitumia mbinu za
udanganyifu ikiwemo kutumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina mengine ili
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kwa upande wa makosa ya Usalama barabarani ACP
Mchunguzi alisema, Madereva 56 wameondolewa madaraja na kufungiwa leseni zao
kwa muda kutokana na makosa mbalimbali ya barabarani na wengine wakilipa faini
Mahakamani kwa makosa ya ukiukaji wa Sheria za Usalama barabarani.
Aidha kwa kipindi cha Novemba hadi Disemba
18,2024 Jeshi la Polisi Mkoani Tanga katika operesheni zake za kuimarisha doria
na misako imewakamata Watuhumiwa 95 wakiwa na makosa mbalimbali ukiwemo
uvunjaji,kujeruhi,wahamiaji haramu na kupatikana na dawa za kulevya .
Katika kudhibiti matukizi ya dawa za kulevya kwa
kipindi cha Novemba hadi Disemba 2024 Polisi umekamata dawa za kulevya aina ya
Mirungi Kg 529 .49 ,bhangi Kg 563, na Pombe ya Moshi Lita 179.5.
Vilevile wahamiaji haramu watatu kutoka nchini
Ethiopia wamekamatwa, mali mbalimbali za wizi ikiwa ni pamoja na televisheni 10
aina mbalimbali, pikipiki Sita aina mbalimbali,fridge mbili aina ya Rock rangi
nyeupe, simu 30 za smart phone na simu ndogo 07,na madumu ya mafuta ya Kula 864
yaliyoingizwa kwa njia ya magendo ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa watuhumiwa
wa matukio hayo.
Jeshi la Polisi Mkoani Tanga linatoa onyo kwa wananchi wote wanaojishughulisha na makosa ya jinai na makosa ya kimtandao kuwa hawataachwa salama bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria.





.jpg)




No comments