POLISI KANDA MAALUMU YA DAR ES SALAAM KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI KUKOMESHA UHALIFU
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Muliro Jumanne Muliro akitoa taarifa ya matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyofanyika wakati wa sherehe za Krisimasi na Mwaka Mpya.
.......................................
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam litaendelea kushirikiana na
wananchi ili kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi kwa ajili ya kupata taarifa
mbalimbali za kihalifu na kuwabaini watuhumiwa sanjari na kuwakamata.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 2, 2025 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Muliro Jumanne Muliro wakati akitoa taarifa ya
matukio ya uhalifu na madereva kuendesha vyombo vya moto wakiwa
wamelewa katika kusherehekea sikukuu za krisimasi na mwaka mpya alisema
mafanikio hayo waliyoyapata yametokana na ulinzi shirikishi.
Alisema jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewafungia leseni za
udereva madereva kadhaa waliokamatwa wakiendesha magari yao huku wakiwa na
kiwango kikubwa cha ulevi jambo ambalo ni kosa kisheria.
Alisema madereva hao wamefungiwa kuendesha magari kwa muda wa miezi sita na
kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa kifungu 28 (3) (b) cha Sheria ya Usalama
Barabarani Sura 168 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.
"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam katika kusherehekea Krismasi
na Mwaka Mpya tulijipanga vizuri na kuweka usimamizi madhubuti wa Sheria na
kanuni mbalimbali zikiwemo za usalama barabarani ili kudhibiti ajali za
barabarani," alisema Muliro.
Muliro alitaja makosa hatarishi ambayo yangepelekea ajali yalidhibitiwa na
kuchukiliwa hatua kwa wahusika ambapo jumla ya madereva 179 walipimwa ulevi
kati yao madereva 30 walikutwa na ulevi wa kiwango cha zaidi ya milligramu 80.
Alisema madereva 22 walikamatwa Wilaya ya Kinondoni, Madereva sita (6)
Wilaya ya Ilala na madereva wawili (2) Wilaya ya Temeke.
SACP Muliro alisema katika kipindi cha Novemba hadi Desemba 2024, Jehi hilo
lilifanikiwa kupata matokeo mahakamani ya watuhumiwa mbalimbali ambapo Sadick
Foreni (30) mkazi wa Mbagala katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke alihukumiwa
kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti huku Joseph Ferdinand (35) mkazi
wa Mbagala Kibonde Maji akifungwa maisha
jela kwa kosa la kulawiti.
SACP Muliro amebainisha kuwa, Ayub Hatibu (32) mkazi wa Tabata alihukumiwa
na Mahakama ya Wilaya ya Kinyerezi miaka
30 jela kosa la kubaka huku Salmin Athuman (30) makazi wa Kitunda akihukumiwa
kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.
Ameongeza Henry Peter (36) mkazi wa Mezi alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya
ya Ubungo miaka 30 jela kwa kosa la kubaka huku Ramadhan Amir (30) mkazi wa
Kawe akihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kifungo cha miaka 30
jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.
Aidha, Kamanda Muliro alisema jumla ya watuhumiwa 250 walikamatwa kwa
kuhusika na kuuza, kusafirisha na kutumia Dawa za Kulevya.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari Elizabeth Pascal mkazi wa
Kipunguni Mashariki Kata ya Ukonga na Patrick Emmanuel walipata fursa ya kutoa
ushuhuda wa jinsi jeshi hilo la Polisi Kanda ya Dar es Salaam walivyofanikiwa
kukamata vifaa vyao vilivyokuwa vimeibwa kwenye nyumba zao pamoja na wahusika.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Muliro Jumanne Muliro akionesha waandishi wa habari moja ya TV iliyokamatwa baada ya kuibiwa.
Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.
No comments