Breaking News

ATE YATOA MSAADA WA MASHINE ZA KUSAIDIA KUPUMUA WATOTO WACHANGA

    Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimetoa msaada wa mashine za kusaidia upumuaji kwa watoto wachanga ambao hupata matatizo ya kupumua mara baada ya kuzaliwa. Msaada huo, uliotolewa mwishoni mwa wiki, unakusudiwa kuokoa maisha ya watoto wachanga na kuimarisha huduma za afya katika hospitali za pembezoni mwa mkoa wa Dar es Salaam.

Mashine hizo, zenye thamani ya shilingi milioni 23, zimetolewa kwa njia ya michango binafsi ya wahitimu wa kozi ya "Mwanamke Kiongozi" awamu ya kumi, inayoendeshwa na ATE. Wahitimu hao, waliotoka taasisi mbalimbali ambazo ni wanachama wa ATE, walichangia fedha za kununua mashine hizo ili kusaidia hospitali zinazokabiliana na changamoto.

Msaada huo ulitolewa katika Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama hicho, Bi. Suzzane Ndomba, ambapo alisema kuwa kiongozi au mwajiri bora ni yule ambaye anajua jukumu lake la kurudisha sehemu ya faida anayopata kwa jamii inayomzunguka na kusisitiza umuhimu wa kuwajibika kwa viongozi na wafanyabiashara katika kuchangia maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Dkt. Jonas Lulandala, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, alibainisha kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mbagala Rangi Tatu inahudumia wagonjwa zaidi ya 1,200 kwa siku na kuwa na mahitaji makubwa ya vifaa vya matibabu.

Alisema kuwa kwa siku zaidi ya watoto 40 wanazaliwa katika hospitali hiyo, na wengi wao hukutana na changamoto za kupumua mara baada ya kuzaliwa. Kwa hivyo, upatikanaji wa mashine hizo za kusaidia upumuaji utasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuimarisha huduma za afya.

Alizungumza kwa niaba ya wahitimu wa kozi, Rais wa Program ya Mwanamke Kiongozi awamu ya Kumi, Adeline Mushi alisema kuwa msaada huo wa mashine za kusaidia upumuaji utakwenda kunufaisha hospitali tano za pembezoni, ikiwa ni pamoja na Sinza Palestina (mashine mbili), Mbagala Rangi Tatu (mashine tano), Kigamboni (mashine moja), Kivule (mashine moja), na Chanika (mashine moja).

No comments