RUTO: NI NJIA YA DIPLOMASIA PEKEE ITALETA AMANI CONGO DRC
Jiji la Dar es Salaam limeandaa
mkutano muhimu uliowakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa lengo la
kujadili suluhu ya kidiplomasia kwa mgogoro wa muda mrefu nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mwenyekiti wa EAC, Rais wa
Kenya Dk. William Ruto, alisisitiza kuwa amani ya kudumu DRC inaweza kupatikana
kupitia njia za mazungumzo badala ya matumizi ya nguvu za kijeshi.
“Historia ya DRC imejaa
changamoto za muda mrefu. Huu ndio wakati wa viongozi kuchukua hatua madhubuti.
Mazungumzo ya kidiplomasia ni suluhisho bora kuhakikisha umoja na amani ya
kudumu nchini humo,” alisema Rais Ruto wakati wa hotuba yake ya ufunguzi
iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Rais Ruto alieleza kuwa vita
vya DRC vimesababisha madhara makubwa kwa wananchi, ikiwemo mamilioni ya watu
kuhama makazi yao, watoto kushirikishwa katika makundi ya waasi, na kuzorota
kwa shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
SADC na Rais wa Zimbabwe, Dk. Emerson Mnangagwa, alitoa wito wa mshikamano
miongoni mwa nchi za Afrika, akilinganisha changamoto za DRC na harakati za
ukombozi wa bara hilo.
“Mgogoro wa DRC unapaswa
kuwaunganisha Waafrika kama ilivyokuwa wakati wa harakati za uhuru. Umoja wetu
ni muhimu katika kuhakikisha usalama na ustawi wa wananchi wa nchi hiyo,”
alisema Rais Mnangagwa.
Mwenyeji wa mkutano huo, Rais
Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa,
Ulinzi na Usalama ya SADC, alieleza kuwa ni jukumu la viongozi wa EAC na SADC
kuhakikisha mgogoro huo unamalizika kwa manufaa ya wananchi wa DRC.
“Wananchi wa DRC wanateseka.
Wameshindwa kushiriki shughuli za kijamii na kiuchumi kwa muda mrefu. Huu ni
wakati wa kufungua ukurasa mpya wa amani na ustawi wa wananchi hao,” alisema
Rais Samia.
Mkutano huo, ambao pia
ulihudhuriwa na viongozi kama Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Yoweri Museveni
wa Uganda, na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, ulilenga kutafuta mbinu
shirikishi kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa na mashirika ya kiraia kuleta
amani ya kudumu DRC.
Viongozi hao waliweka bayana kuwa ushirikiano
wa kanda hizo mbili ni muhimu katika kuhakikisha mzozo wa DRC unashughulikiwa
kikamilifu kwa kutumia njia za kidiplomasia.Marais wakiwa kwenye kikao hicho
Taswira ya kikao hicho
No comments