Breaking News

SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU, VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akisaini kwenye kitabu cha wageni Februari 08, 2025 mkoani Iringa wakati akizindua jengo la Bwalo la Chakula katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha.

................................................. 

Na Mwandishi Wetu, Iringa 

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kujikita katika ukarabati wa miundombinu chakavu na ujenzi wa miundombinu mipya na ya kisasa kwa ajili ya taasisi za mafunzo nchini hususani Vyuo vya Maendeleo ya Jamii. 

Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo Februari 08, 2025 mkoani Iringa wakati akizindua jengo la Bwalo la Chakula katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha. 

Naibu Waziri Mwanaidi amesema Chuo cha Mendeleo ya Jamii Ruaha ni miongoni mwa Taasisi za mafunzo zilizonufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, ambapo  ametoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Jengo la Utawala, Bweni la Wasichana  pamoja na Jengo la Kituo cha Ubunifu na Maarifa. 

Ameongeza kwamba, Serikali imetoa  fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, maktaba, ukumbi wa mihadhara pamoja na bwalo la chakula la kisasa ambayo kwa pamoja yameongeza wigo wa utoaji wa huduma za elimu chuoni hapo.

 

Amesema Mwaka 2022/23 Serikali ilitenga kiasi cha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo kwa lengo la kutatua changamoto iliyokuwa inawakabili wanafunzi ya kukosa sehemu nzuri ya kupatia huduma ya chakula.   

"Ninawasihi tuungane na kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake sikivu kwa kuondoa kadhia iliyokuwa inawakabili wanafunzi kwa muda mrefu. Nina amini kuwa bwalo hili litaongeza tija ya kuinua taaluma ya Chuo hiki kwa kuwawezesha wanafunzi kupata huduma ya chakula katika mazingira salama, rafiki na kwa wakati" amesema Naibu Waziri Mwanaidi. 

Mhe. Mwanaidi ametoa rai kwa Jumuiya ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kuhakikisha kuwa wanatunza miundombinu yote ya Chuo hicho hususani bwalo la chakula na kuhakikisha lengo la Serikali la kujenga miundombinu rafiki ya kutolea huduma ya elimu kwa Wananchi linatimia kikamilifu kama ilivyokusudiwa. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Doris Kalasa ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kukiwezesha Chuo hicho kuboresha miundombinu mbalimbali inayohusika na kujifunza na kujifunzia ili kuendana na mabadiliko ya utoaji wa elimu hasa katika mabadiliko ya Teknolojia. 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha Godfrey Mafungu amemuhakikishia Naibu Waziri Mwanaidi kuwa atasimamia vyema utunzaji wa miundombinu mbalimbali Chuoni hapo ili idumu na kunufaisha wanafunzi watakaosoma vizazi kwa vizazi.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la Bwalo la Chakula katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha. 
 

No comments