BUNGE LAIPONGEZA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeipongeza Wizara
ya Maliasili na Utalii kwa mafanikio iliyoyapata katika kukuza utalii huku
likiipitisha taarifa ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii
kuhusu shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha Februari,2024 hadi Januari,
2025.
Akizungumza katika Mkutano wa 18, Kikao cha 9 cha Bunge hilo
leo jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ametoa pongezi hizo na kuielekeza Wizara
hiyo kuendelea kufanya maboresho hasa kwenye utaratibu wa makusanyo ya mapato
ya taasisi za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili
kurahisisha shughuli za uhifadhi ikiwemo ukarabati wa miundombinu ndani ya
maeneo ya hifadhi.
Aidha, Mhe. Mnzava ameitaka Wizara hiyo kuendelea kugundua
mazao mapya ya utalii sambamba na kutangaza vivutio vya utalii nchini kwa njia
ya kidijitali.
Kuhusu kuboresha huduma za malazi kwa watalii, Mhe.
Mzava ameitaka Wizara ya Maliasili na
Utalii kufanya tathmini ya hoteli na lodges za Serikali zilizobinafsishwa kwa
wawekezaji kwa lengo la kusimamia mapato na taratibu za uendeshaji wake.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi
Chana (Mb) amesema kuwa chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Sekta ya Utalii imekua ukilinganisha
na kipindi cha kabla ya janga la Uviko 19.
“Tumefanikiwa kuongeza idadi ya watalii mpaka sasa tumefikia
watalii milioni 5.3 na mapato yatokanayo na utalii yamefikia dola za kimarekani
bilioni 3.6” amesisitiza Mhe. Chana.
Mhe. Chana ameweka bayana kuwa Serikali itaendelea kuboresha
miundombinu na huduma za malazi katika maeneo ya hifadhi na kwamba mpaka sasa
Shirika la UNESCO limetoa kibali cha
kuridhia ujenzi wa barabara ya tabaka gumu kutoka Nabi hadi Fort Ikoma katika
eneo la Ngorongoro.
Kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa dunia wa Ufugaji
Nyuki (APIMONDIA) 2027 amefafanua kuwa mpaka sasa limepatikana eneo lenye ukubwa wa ekari 48
kwa ajili ya mkutano huo na mchakato wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi
unaendelea.
No comments