GBP YAWEKEZA DOLA 50 MILIONI UJENZI WA MRADI LPG TERMINAL GBP TANGA
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aipa Kongole GBP, Aitaka Kukamilisha Haraka Mradi wa Ujenzi wa Ghala la Kuhifadhi Nishati Safi LPG Terminal Tanga.
.jpg)
Na Mashaka Kibaya, Tanga
........................................
KAMPUNI ya GBP ya Jijini Tanga imewekeza dola milioni 50 kwa lengo la kutekeleza mradi wa ujenzi wa ghala la kupokea na kuhifadhi gesi (LPG Terminal), ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mnamo Machi Mosi mwaka huu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi mradi huu kwa kuweka jiwe la msingi, huku akisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea matumizi na upatikanaji wa nishati safi kwa ajili ya kupikia.
Mbali na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema, mradi huu utakuwa msaada mkubwa kwa matumizi ya nishati viwandani, kama ilivyo katika mikakati ya Serikali ya kufungua viwanda vingi, hasa Mkoani Tanga.
Katika taarifa yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mmiliki wa Kampuni ya GBP, Badar Soud, alisema kuwa wamekusudia kufanya mapinduzi makubwa kwenye mpango wa matumizi ya nishati safi. Soud ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa GBP, alieleza kuwa wanapanga kujenga ghala kubwa la kuhifadhi tani 30,000 za gesi safi ya kupikia, huku wakidokeza kwamba matarajio yao ni kuwa terminal hiyo itakuwa kubwa zaidi nchini.
"Tumepanga kujenga terminal kubwa ya tani 30,000, na tunatarajia kuwa itakuwa terminal kubwa zaidi kwa Tanzania," alisema Soud na kuongeza kuwa GBP ina mikakati ya kutumia magari ya kisasa kusafirisha nishati husika kwenda kwa watumiaji katika maeneo mbalimbali.
Aidha, Soud alisema: "Kuhusu LPG, tunakuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa jitihada zako za kuleta mapinduzi ya nishati safi, mradi huu umejikita katika kuboresha maisha ya wanawake barani Afrika kwa kupunguza maradhi yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa."
Soud aliongeza kuwa GBP inakusudia kupanua huduma zake kwa kujenga stesheni za kujazia mitungi ya gesi katika mikoa mbalimbali nchini, na kwamba wanatarajia kutoa ajira zaidi ya 1,000 kwa Watanzania.
Mipango mingine ya GBP ni kuwekeza zaidi Zanzibar, kwenye visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo tayari wamewekeza. Vilevile, walizungumzia mipango ya kujenga kiwanda cha vilainishi na kujenga bandari ya kupokea meli kubwa zaidi.
Kwa upande mwingine, Soud alisisitiza kuwa GBP imefanikiwa kuwa na bohari kubwa ya kuhifadhi mafuta na miundombinu bora ya kupokea, kupakia, na kusafirisha mafuta, huku wakidai kuwa wanaongoza kwa ukubwa wa bohari za kuhifadhi mafuta nchini.
Soud alibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2000 walipoanza, walikuwa wakilipa kodi ya Serikali ya shilingi milioni 600, na hadi sasa wamelipa zaidi ya shilingi bilioni 25 hadi 30 kwa mwezi.
Badar Soud aliipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka misingi imara ya uwekezaji, uchumi, haki, misingi ya sheria, na suala la kudumisha amani nchini Tanzania. Aliipongeza Serikali kwa kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, akisema maendeleo yaliyofikiwa ni matokeo ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Rais Samia.
Soud aliongeza kuwa mkutano wa masuala ya nishati uliowakutanisha marais zaidi ya 20 wa Afrika Jijini Dar es Salaam ni uthibitisho wa uongozi bora wa Rais Dkt. Samia, akimtaja kama kiongozi mwenye maono ya mabadiliko chanya.
Katika hotuba yake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliupongeza uwekezaji huo wa GBP akiwasihi kwa uvumilivu mkubwa waliouonesha katika utekelezaji wa majukumu yao kwa miaka 25 na mafanikio waliyojipatia.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa kampuni ya GBP imekuwa na mafanikio makubwa katika usambazaji wa mafuta katika ukanda wa Kaskazini na kwamba wanastahili kuendelea na kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa. Aliendelea kusema kuwa kuna haja kwa Wizara ya Nishati kuangalia namna ya kusaidia waendeshaji wa sekta hiyo, akiwataja GBP kuwa na bohari kubwa ya kuhifadhia mafuta.
Kuhusu mradi wa LPG Terminal Tanga, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wawekezaji hao kukamilisha mradi huo haraka ili wananchi wa Tanga wapate fursa za ajira. Alisema kwamba ajira 1,500 zinaweza kupatikana na kwenye mradi utakaoleta mzunguko wa fedha kwa wananchi.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwahakikishia wawekezaji wote, wakiwemo wa ndani na nje ya nchi, kuwa Tanzania imefunguka kwa uwekezaji. akiwakumbusha kuwa Tanzania ni nchi salama yenye sera rafiki kwa maendeleo endelevu.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, alisema ,Mkoa wa Tanga ni moja ya maeneo muhimu katika sekta ya nishati na pia ni kitovu cha kupokea mafuta na kusambaza mikoa iliyopo Kanda ya Kaskazini.
Kapinga alisisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea ni matokeo ya sera nzuri za Serikali zinazovutia wawekezaji na kusaidia ajenda ya nishati safi ya kupikia, huku akifafanua kuwa hadi kufikia mwaka 2030, Watanzania wote wanapaswa kufikia nishati safi kwa ajili ya kupikia.
No comments