Breaking News

MADIWANI KILINDI KUTUMIA MUDA ULIOBAKI KUKAMILISHA MIRADI

Madiwani Kilindi watumia muda uliobaki kukamilisha miradi viporo.

DC Kilindi ahimiza umuhimu wa kuhifadhi chakula, ataka makusanyo ya Serikali kupanda.

Mikutano ya taarifa za mapato na matumizi vijijini kuwa indiketa Viongozi wanawajibika kwa Wananchi.

 Mkuu wa wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa.akizungumza kwene kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi Aprili 18, 2025 mkoani Tanga.

......................................................

Na Mashaka Kibaya, Kilindi 

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga wametakiwa kutumia kipindi kichosalia kuhakikisha miradi iliyopo ikiwemo Ile ya viporo inakamilika kwa asilimia 100% ili kuweza kuwanufaisha wananchi.

Rai hiyo imetolewa Jana na Mkuu wa wilaya hiyo Hashim Mgandilwa alipokuwa akiwasilisha Salaam za Serikali kwenye kikao cha madiwani cha robo ya tatu, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo ya Wananchi.

"Nitumie fursa hii kumshukuru Rais kwa usimamizi na kuleta fedha nyingi za miradi. Waheshimiwa Madiwani twendeni tukasimamie miradi hasa ile viporo katika kipindi kilichosalia ifike asilimia mia moja kabla ya mabaraza kuvunjwa" alisema Mgandilwa.

Licha ya hayo Mkuu huyo wa wilaya pia aliwataka Wajumbe hao wa baraza  la madiwani kuwaelimisha wananchi kuhifadhi chakula na kuacha tabia ya kuuza mazao kiholela ili 
 kuweza kujikinga na changamoto ya uhaba wa chakula pindi ikijitokeza.

Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akielezea wasiwasi wake juu ya kujitokeza kwa changamoto ya upungufu wa chakula kutokana na mvua za mwaka huu kukosa kueleweka hivyo kuathiri msimu wa kilino.

"Mwaka huu tumepata changamoto ya mvua, tulizoea kuvuna awamu mbili na zinaweza kukosekana. Kumekuwa na tabia ya kuuza sana mazao yetu hivyo viongozi tuwaelimishe Wananchi kuhifadhi, itakuwa aibu kwa Kilindi kulalamika chakula" alisema Mgandilwa.

Mbali na kuwazungumzia Wananchi wa kawaida pia Mgandilwa aliwataka wafugaji kujiwekea hifadhi ya chakula baada ya kuuza mifugo yao badala ya kutumia fedha waliyozipata kwenye mambo ya anasa.

"Wafugaji wamekuwa na tabia ya kuuza ng"ombe kwenye minada, wakipata fedha wananunua vindama vya kufuga tena na hela zinazobaki wanachoma nyama huku wakinywa pombe hii siyo sawa vyema mtu akipata fedha anunue debe la mahindi" alisema.

Katika salaam zake hizo Mkuu huyo wa wilaya pia aliwahimiza Madiwani na watendaji kushirikiana na kuongeza juhudi kwenye suala zima la ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Pia Mkuu huyo wa wilaya amekumbusha umuhimu wa kufanyika kwa mikutano ya utoaji wa taarifa za mapato na matumizi kwenye vijiji, kwa madai kuwa kufanya hivyo kuwa na Serikali zinazoweza kuwajibika kwa wananchi.

Vile vile DC Mgandilwa aliwasihi madiwani kusaidia kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo yao, aliwasihi kuanza na migogoro ya mipaka ya kijiji kwa Kijiji akishauri kushawishi maridhiano njia ya amani.

Wakati Mgandilwa alisema hayo, Mwenyekiti wa CCM wilayani Kilindi Rajabu Kumbi amerejea kuwasisitiza Madiwani kwenda kutatua migogoro ya ardhi akiwaasa kuacha kutafuta kura kwa kutengeneza migogoro.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Kilindi Idirisa Mgaza aliishauri Serikali ya wilaya hiyo kupitia Mkuu wake wa wilaya kwenda kuketi na Kiongozi mwenzake wa Handeni ili kumaliza tofauti za mipaka zoezi ambalo tayari lilifanyiwa kazi.

Mgaza alisema,kuna mgogoro ambao tayari ulishughulikiwa na kilichosalia ni wakuu wa wilaya za maeneo husika kukutana ili kubainisha kwa wananchi maamuzi yaliyofikiwa ili kumaliza utata wa awali jambo ambalo halijafanyika.

Katika Mkutano huo wa baraza la madiwani alikuwepo katibu wa CCM Asha Jumanne Mwendwa aliyehamia wilayani Kilindi akitokea Lindi ambapo alitumia fursa hiyo kujitambukisha huku akiomba ushirikiano.
Katibu wa CCM Wilaya a Kilindi, Asha Mwendwa, akichangia jambo kwene kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi,  Idirisa Mgaza.akiongoza kikao hicho.

Mwenyekiti wa CCM wilayani Kilindi Rajabu Kumbi, akizungumza
Kikao hicho kikiendelea
Madiwani wakiwa kwene kikao hicho.

Kikao kikiendelea
 

No comments