Breaking News

PATRICK MITRI ANAVYOWIWA KUTUMIA KIPAJI CHAKE KUSAIDIA JAMII IONDOKANE NA UMASIKINI

 # Ajipanga kutumia vijiwe vya Kahawa kusaka suluhu ya umasikini hapa nchini.

Na Mwandishi Wetu,Tanga.

KATIKA kijiji kidogo chenye utulivu wa asili kiitwacho Mgila, ndani ya Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, anapatikana Patrick George Mitri mwanaharakati wa kipekee  asiye wa kawaida, bali ni mtu aliyejitoa kwa dhati kulikomboa taifa dhidi ya adui umasikini. 

Ni kupitia kipaji chake alichokigundua mwaka 2000 na kukianza rasmi mwaka 2003, Patrick ameibuka kama sauti ya matumaini kwa Watanzania, hasa wale wenye kipato cha chini.

Patrick anasema kwamba harakati zake hazikutokana na msukumo wa kisiasa au dini, bali ni mwitikio wa kiroho na dhamira binafsi aliyepewa kupitia kipaji alichogundua ndani yake.

 Kwa kipindi kirefu alitafakari juu ya changamoto zinazolikabili taifa, na baadaye, aliamua kuchukua hatua ya kuanza safari ya kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.

Lengo kuu ya harakati zake ni kupambana na hali ya umasikini unaowaandama Watanzania walio wengi, anakusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi yatakayonufaisha mtu mmoja mmoja hata bila kusubiri neema toka juu.

 Kwa Patrick, ukombozi wa taifa hautaanzia kwa mabadiliko ya sera pekee, bali kwa mabadiliko ya fikra na mtazamo wa maisha.

Tofauti na wanaharakati wengine, Patrick amesisitiza kwamba, harakati zake si za kisiasa, kidini wala kikabila. Anapinga kabisa kutumia jukwaa hili kwa ajili ya kujinufaisha au kujipatia umaarufu. Analenga utaifa.

 Kusimama kama Mtanzania anayetaka kuona mabadiliko ya kweli kwa watu wote bila ya kuwepo kwa ubaguzi.

Kabla ya kuanza rasmi harakati zake, Patrick anasema kwamba anakusudia kukutana na viongozi wa kitaifa. Anawahitaji viongozi wa serikali, akiwemo Rais pamoja na viongozi wa dini kutoka madhehebu yote, ili kuwaeleza dhamira yake na kuomba ushirikiano wao.

Anaamini kwamba bila baraka na msaada wao, harakati hizi haziwezi kuwa na mafanikio ya kudumu.

Patrick anapanga kuanza harakati zake kwa kipindi cha ukimya anachokiita 'Silent Time'. Katika kipindi hiki, atazunguka kwenye vijiwe vya kahawa, vijiwe ambavyo ni vyuo visivyo rasmi vya maarifa kwa jamii. Huko atakutana na wananchi wa kawaida, wadau, na wanafikra kubadilishana mawazo na kuandaa msingi imara wa harakati zake.

Anaona vijiwe vya kahawa kama mahali muhimu pa kujenga hoja na kupima mitazamo. Katika vijiwe hivyo, watu hujadili mambo kwa uhuru na kutoa maoni bila woga. Patrick atavitumia kama jukwaa la awali la kueneza fikra zake na kuvuta hisia za watu wa kawaida wanaohusika moja kwa moja na mapambano ya vita dhidi ya umasikini.

Patrick anasisitiza kuwa mabadiliko hayawezi kuletwa na mtu mmoja. Anawaalika Watanzania wote kushiriki, bila kujali tofauti zao. Harakati zake ni za umoja, mshikamano, na kujitambua – kwa vile kila mmoja wetu anao wajibu wa kushiriki katika kuijenga nchi ama Taifa.

Kipaji alichonacho si cha kawaida. Anaeleza kuwa ni uwezo wa kuona mbali, kuunganisha fikra na kujenga mifumo mbadala ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo katika jamii. Hiki ndicho anachotaka kukifanya kwa vitendo.

Patrick yupo tayari kujitolea kwa ajili ya harakati hizi. Anasema hawezi kurudi nyuma kwa sababu anaamini alichonacho si kwa ajili yake peke yake, bali kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Anaamini hakuna mtu anayestahili kuishi katika lindi la umasikini kwenye nchi yenye utajiri wa rasilimali kama Tanzania.

Anatambua kwamba harakati hizi hazitakosa vikwazo. Kutokueleweka, upinzani kutoka kwa baadhi ya watu wenye maslahi binafsi, na ukata ni baadhi ya changamoto anazotarajia. Hata hivyo, anaamini kuwa kwa msaada wa wananchi na viongozi, kila changamoto inaweza kushughulikiwa.

Anatoa wito kwa serikali kushirikiana na wanaharakati wa aina yake. Serikali iwe tayari kusikiliza mawazo mbadala na kuwapa nafasi watu wenye dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo. Viongozi wa dini pia wasimame kama nguzo ya maadili katika harakati hizi.

Maono ya Patrick ni kuona jamii ya Watanzania iliyojitegemea, yenye uchumi imara unaotokana na juhudi za watu wenyewe. Anaamini tunaweza kujenga taifa ambalo wananchi wake si wahitaji wa msaada, bali washirika wa maendeleo.

Katika zama hizi ambapo wengi wamekata tamaa au kuangukia siasa za maneno matupu, Patrick George Mitri anasimama kama mfano wa kuigwa. Harakati zake ni mwanga katika giza la umasikini, mwanga unaoanza kuwaka kijijini Mgila lakini wenye uwezo wa kuangaza taifa zima. Kama watapata sapoti anayohitaji, huenda historia ya kupambana na umasikini Tanzania ikaandikwa upya.


 

No comments