TMA YATOA TAHADHARI KWA WANANCHI KIPINDI CHA JUNI HADI AGOSTI 2025



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi Dkt. Ladslaus Chang’a (katikati)  akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mei 22, 2025 alipokuwa akitoa taarifa ya muelekeo wa hali ya hewa katika kipindi cha Juni hadi Agosti 2035. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma ya Utabiri TMA Dkt. Changa na Kulia ni Mtaalam wa Hali ya Hewa wa TMA, Omary Ramadhani.

.......................................


Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) imetoa ushauri kwa wananchi kuchukua tahadhari za kiafya katika kipindi cha mwezi cha Juni hadi Agosti ambacho kitatawaliwa na hali ya baridi.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi Dkt. Ladslaus Chang’a wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mei 22, 2025 ambapo alihimiza wadau mbalimbali watumie taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi cha Juni hadi Agosti kutokana na  kutawaliwa na hali ya baridi.

 “ Kipindi hicho maeneo mengi yanatarajiwa kupata baridi kali na vumbi hivyo wafugaji wanashauriwa kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo na kufuata ushauri wa wataalamu, huku wakulima wakihimizwa kutumia maeneo oevu kwa kilimo cha mazao ya muda mfupi kama mbogamboga na viazi,” alisema.

Aidha, alisema watumiaji wa shughuli za baharini wanatakiwa kufuatilia utabiri wa kila siku na angalizo kuhusu upepo mkali kwa usalama wao.

Akizungumzia msimu huo Chang’a alisema hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi  na kuwa hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Dodoma.


Alisema mwezi Julai ndio kipindi cha baridi zaidi, huku maeneo yenye miinuko ikitarajiwa kushuka chini ya nyuzi joto 6°C, hasa katika nyanda za juu kusini-magharibi.

Aidha amesema vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai na vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, ukanda wa mwambao wa pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Amesema msimu wa kipupwe 2025 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025 katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

TMA imetabiri upepo wa wastani kutoka Kusini Mashariki utakaotawala maeneo mengi, huku vipindi vya upepo mkali kutoka kusini (upepo wa kusi) vikitarajiwa hususan mwezi Juni na Julai, hasa katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya nchi kavu.


Mwelekeo wa Mifumo ya Hali ya Hewa

Kwa mujibu wa TMA, joto la bahari linatarajiwa kuwa la wastani katika maeneo mengi ya tropiki, huku joto la juu ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi likitarajiwa kudhoofisha upepo wa baridi kutoka kusini.

Angalizo

TMA itaendelea kufuatilia hali ya hewa na kutoa taarifa za mara kwa mara. Wananchi na wadau wanahimizwa kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 na mwezi kutoka TMA pamoja na tahadhari zinazotolewa kuhusu hali mbaya ya hewa.

Kwa taarifa zaidi, tembelea tma.go.tz au akaunti rasmi za TMA katika mitandao ya kijamii.


No comments