AHADI HEWA ZA VIONGOZI ZAWACHOSHA WANANCHI KIVULE, MSONGOLA
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ojambi Masaburi akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Litongo Dar es Salaam (ULIDA) ambapo pia alitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa miradi ya barabara katika maeneo ya Kata za Msongola na Kivule.
...............................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WANANCHI wa
Kata ya Msongola na Kivule Ilala Jijini Dar es Salaam wamesema wamechoshwa na
ahadi ambazo zimekuwa zikidaiwa kutolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali kuhusu
ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Watetoa
malalamiko hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na waandishi wa habari
kuhusu kadhia wanayoipata hasa katika kipindi hiki cha mvua aza masika
zinazoendelea kunyesha.
Mkazi wa
Msongola Colman Marwa ambaye ni Mwenyekiti Mstaafu wa Mtaa wa Yangeyange
alisema changamoto ya barabara ni ya muda mrefu hivyo anaiomba Serikali kusikia
kilio cha wananchi juu ya ujenzi wa barabara hizo.
“Mimi nipo
katika eneo ili tangu mwaka 2000 naona barabara ya kutoka njia panda ya Kivule
hadi Kitunda na kipande cha barabara kutoka Msongola hadi Mbande jinsi ambavyo
viongozi wamekuwa wakitoa ahadi za kuzitengeneza lakini hatuoni matokea,”
alisema Marwa.
Alisema hata
mwaka huu barabara hizo zilianza kutengenezwa lakini zimekuwa hazikamiliki huku
kizingizio kikubwa ikiwa ni mvua jambo ambalo limewafanya wananchi wakosema
Imani na ahadi hizo zinazotolewa na viongozi hao.
Mkazi wa
Msongola kwa Chande, Hadija Rajabu alisema kutokana na ubovu huo wa barabara
wanalazimika kulipa nauli mara mbili au zaidi ile ya kawaida.
“ Kutokana
na ubovu wa barabara dereva wa bajaji au bodaboda anapandisha nauli anayoitaka
mfano sehemu tunayopaswa kulipa nauli ya Sh. 500 kwa bajaji kutoka Njia Panda ya
Kivule hadi Fremu Kumi tunatozwa Sh.1000 hadi 1500,” alisema.
Aliongeza
kuwa athari wanazokumbana nao ni wajawazito kuwa katika wakati mgumu
wanapokwenda Hospitali ya Wilaya ya Kivule kujifungua kutokana na
kurushwarushwa kutokana na ubovu huo wa barabara.
Mkazi wa
Msongola ambaye ni dereva wa bodaboda Omari Jafari alisema yupo katika eneo
hilo tangu 2015 na katika kipindi cha Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Pombe
Magufuli aliagiza barabara hizo zikiwekwa kifusi ikiwa ni maandalizi ya
kujengwa kwa kiwango cha lami lakini mpaka leo hii kipande cha barabara kutoka
Msongola hadi Mbande kina hali mbaya na magari yanapita kwa kushida kutoka na
mashimo makubwa na madimbwi ya maji.
Mkazi wa
Yangeyange Waitara Magori alisema kutokana na ubovu wa barabara hizo sehemu
ambayo walipaswa kutumia kwa dakika tano hadi hadi kumi wanatumia zaidi ya nusu
saa hadi saa moja.
Dereva
bodaboda, Dismas James mkazi wa Kivule anasema kutokana na ubovu wa barabara
hizo ameathirika kiafya kwani amekuwa
akipata maumivu ya mgongo.
Diwani wa
Kata ya Msongola, Azizi Mwalile alikiri kuwepo kwa changamoto ya barabara hizo
na kueleza kwamba tayari Serikali imeanza kuzifanyia kazi akitolea mfano ya
barabara ya kutoka Msongola kwenda Kivule imeanza kujengwa na mkandarasi wa
Kampuni ya Jiangxi Geo Engineering ya China kupitia mradi wa DMDP-2.
Kwa upande
wake Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ojambi Masaburi
alisema ni kweli hali ya barabara hizo sio nzuri lakini Serikali imeanza
kuzifanyia kazi barabara hizo na wakandarasi wapo kwenye maeneo ya mradi baada
ya kusaini mkataba wa ujenzi.
“Changamoto
iliyopo hivi sasa ni hizi mvua zinazoendelea kunyesha zinawapa wakati mgumu
wakandarasi na kushindwa kufanya kazi,” alisema Masaburi.
Masaburi alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hizo ambapo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na subira.
No comments