MIRADI ILIYOJENGWA NA WAZAWA YAFIKIA SH. BILIONI 50
1)Waziri wa Ujenzi , Abdallah Ulega akisalimiana na kupeana mikono na washiriki mbalimbali kwenye mkutano huo wa siku pili wa wadau wa sekta ya ujenzi unaoendelea jijini Dar es Salaam.
.....................................................
Na Damas Makangale, Dar es Salaam,
SERIKALI ya awamu ya sita chini Dkt Samia Suluhu Hassan imetekeleza kwa vitendo miradi ya upendeleo kwa makandarasi wa ndani kutoka Tsh bilioni 10 hadi Tsh bilioni 50 katika juhudi za kuwajengea uwezo wazawa hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Hamis Ulega Wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na wadau wa sekta ya ujenzi jijini Dar es Salaam, alisema kwamba hayo ni matokeo ya serikali kuyafanyia kazi maazimio ya wadau yaliyotokana na mikutano kama hiyo.
Alisema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha makandarasi wa ndani kukua na kutekeleza sehemu kubwa ya miradi ya ujenzi inayotekelezwa hapa nchini na hata kuweza kushindana katika masoko ya nje ya Tanzania.
Aliongeza Kwamba hiyo itasaidia sehemu kubwa ya faida itokanayo na miradi ya ujenzi kubaki hapa nchini kwa manufaa ya uchumi wa nchini lakini pamoja na mambo mengine kuongeza mapato ya fedha za kigeni kwa miradi ya nje ya Tanzania.
“Aidha, Mwenyekiti wa Bodi, kupitia hotuba yake ya kunikaribisha, ameipongeza Serikali kwa kutoa kipaumbele kwa makandarasi wa ndani kupitia vifungu wezeshi katika sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024”, alisema Ulega
Ulega aliongeza kwamba serikali itaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha malipo ya makandarasi yanalipwa kwa wakati kwa sababu ucheleweshaji huo unaathiri huduma kwa wananchi.
“Serikali inafanya kila jitihada kupata fedha za kulipa makandarasi na kila mara fedha zinapopatikana, kipaumbele kinatolewa katika kulipa madeni ya makandarasi wa ndani,’ alifafanua Ulega.
Waziri Ulega alitoa wito kwa waajiri nchini kuruhusu matumizi ya dhamana za bima katika shughuli za mbalimbali kwenye sekta ujenzi ili kupanua wigo kwa wakandarasi kuchagua dhamana za benki na bima.
“Wito wangu ni kwa waajiri wote kutambua kwamba mazingira ya sekta ya bima kwa sasa yameboreshwa sana na ipo mamlaka ya usimamizi wa bima nchini (Tanzania Insurance Regulatory Authority - TIRA), hivyo wasiwe na mashaka katika kuruhusu matumizi ya dhamana za bima kwenye sekta hii muhimu,” alisema .
Alisisitiza umuhimu kwa makandarasi kuzingatia weledi na uzalendo katika shughuli za ukandarasi pamoja na kutekeleza miradi kwa wakati na kwa viwango vya ubora kulingana na mikataba ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa na Thamani ya Fedha iliyokusudiwa (Value for Money).
“Mtambue kwamba sekta yetu ya ujenzi ina mchango mkubwa sana katika kuzifanya sekta zingine za kiuchumi kufanya vizuri kupitia miundombinu mbalimbali,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Mhandisi Joseph Nyamhanga aliipongeza serikali kwa kuwezesha utungwaji wa sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024 kwa kuzingatia ukuaji wa makandarasi wa ndani.
“Kwa mfano, sheria imeelekeza miradi yote isiyozidi TZS 50 bilioni na ikiwa inatekelezwa kwa fedha za ndani, ishindaniwe na kutekelezwa na makandarasi wa ndani pekee. Mheshimiwa Mgeni Rasmi, hili likitekelezwa ipasavyo, litatoa fursa kubwa kwa makandarasi wa ndani kukua.”
“Yapo mengine mengi mazuri katika sheria hiyo mpya na kanuni zake kama vile waajiri kutenga miradi maalum ya kukuza uwezo wa makandarasi wa ndani, kutoa upendeleo maalum (margin of preference) kwa mzabuni wa ndani anaposhindana na mzabuni wa kigeni au kwa mzabuni mwenye ubia baina ya kampuni ya ndani na ya kigeni, pamoja na kampuni za kigeni kutakiwa kuwa na ushirika au mikataba midogo na kampuni za ndani..” alisema Mhandisi Nyamhanga.
Mwenyekiti huyo wa Bodi aliwaasa makandarasi wajiepushe na vitendo vya rushwa kwa kukataa kushawishi na kushawishiwa kutoa rushwa na washindane kwa haki ili kupitia mchango wao kama makandarasi, wakuze uchumi wa nchi yao na pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuungana na kufanya kazi kwa ubia (Joint Venture) kila zinapojitokeza fursa za miradi mikubwa hapa nchini.
Naye Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Rhoben Nkori alisema mkutano huo ni fursa ya mashauriano ni jukwaa linalounganisha wadau wa sekta ya ujenzi kutoka serikalini na sekta binafsi wakiwemo waajiri, makandarasi, wataalam washauri na wengineo kukutana kwa ajili ya kupeana taarifa, kushauriana, kujitathimini na kuweka mikakati madhubuti kwa ajili ya kuboresha shughuli za ujenzi hapa nchini.
Kaulimbiu katika mkutano huo wa mashauriano kwa mwaka 2025 ni “Ukuaji wa Makandarasi wa ndani; Fursa na changamoto” katika .ukuaji wa Makandarasi wa ndani kwa maslahi mapana ya nchini.
Waziri wa Ujenzi , Abdallah Ulega akisalimiana na kupeana mikono na washiriki mbalimbali kwenye mkutano huo wa siku pili wa wadau wa sekta ya ujenzi unaoendelea jijini Dar es Salaam
Post Comment
No comments