MSAMA AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUTOJIHUSISHA NA SIASA KWENYE NYUMBA ZA IBADA

Mkurugenzi wa Msama Promotions,  Alex Msama, akizungumza na waandishi wa habari Juni 8, 2025 Jijini Dar es Salaam na kueleza kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wa dini ambao wanatumia nyumba za ibada kufanya siasa.

...............................................

Na Mwandishi Wetu

VIONGOZI wa dini wametakiwa kuacha kutumia nyumba za ibada kufanya siasa na kuwa kazi hiyo waachie wana siasa wenyewe.

Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Msama Promotions Alex Msama wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kueleza kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakifanya hivyo.

“Vyombo vya dola vichukue hatua kali dhidi ya viongozi wa dini ambao wanatumia makanisa na misikiti kuzungumzia masuala ya siasa badala ya kuhubiri neon la Mungu,” alisema Msama.

Msama akizungumza katika mkutano huo huku akinukuu baadhi ya vifungu kutoka katika biblia Takatifu kitabu cha warumi aliwataka viongozi hao kuheshimu mamlaka zilizowekwa na Mungu na kueleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo katika nafasi hiyo baada ya kuwekwa na Mungu hivyo kumdhihaki na kumtukana ni kukinzana na Mungu.

“Kitabu cha warumi 13 mstari wa pili kinaeleza kuwa amuasie mwenye mamlaka anashindana na agizo la Mungu hivyo mambo ya siasa waachiwe wanasiasa kwani mtu hawezi kuwatumikia mabwana wawili lazima atampenda mmoja na mwingine atamchukia,” alisema Msama,

Aliongeza kuwa kila  kiongozi wa dini anayechanganya dini na siasa anachokitafuta ndicho atakivuna hivyo anapokutana na mkono wa dola asilalamike wala kumtupia mtu lawama badala yake atubu na kumuomba msamaha Rais ambapo aliwaomba wafanye kazi ya Mungu na wasiingiwe na roho za tamaa za kishetani.

“Kafanyeni kazi ya kuwavuta watu kutoka kwa shetani na kuwaleta kwa Mungu kwa kuyacha matendo yote maovu yakiwemo ya kuvuta bange,” alisema Msama.

Mkurugenzi wa Msama Promotions Alex Msama akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
 

No comments