SIMBA TERMINAL YAANZA KUFUFUA ZAO LA MINAZI TANGA
Wananchi wakipokea miche ya minazi kutoka Kampuni ya Simba Terminal ya Mkoa wa Tanga.
Mashaka Kibaya, Tanga.
KAMPUNI ya Simba Terminal imegawa miche ya zao la minazi kwa wakazi wa vijiji vitano (5) vya Kata ya Gombero Wilayani Mkinga Mkoani Tanga lengo likiwa kufufua Kilimo hicho na kuimarisha Uchumi kwa Wananchi.
Hatua hiyo umekuja ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kusaidia maendeleo ya jamii, ambapo Meneja miradi wa Simha Terminal Innocent Tirya alisema jana kuwa miche hiyo ya minazi itagaiwa kwa awamu mbili.
Katika zoezi hilo la ugawaji wa miche hiyo 3000 lililosimamiwa na wenyeviti wa vijiji vya Gombero, Kivuleni, Mgandi, Jirini Bombo na Jirini Mfuduni Wakazi wake walielezea matumaini yao ya kuimarisha Uchumi wa familia zao kupitia minazi.
Katika taarifa yake Meneja wa Simba Terminal Innocent Tirya alisema, kampuni yake chini ya Simba Bingwa imekuwa na utaratibu wa kuchangia maendeleo ya kijamii kutokana na faida inayopata ikiwa sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuharakisha maendeleo kwa umma.
Alisema kwamba, Simba Terminal katika mradi huo unaotekeleza Kata ya Gombero itasambaza miche ya minazi 5,000 ambayo imeshainunua ambapo awamu ya kwanza wamegawa miche 3,000 huku awamu ya pili ikikusudia kugawa 2,000 mgeni rasmi atakuwa mkuu wa mkoa wa Tanga Dkt Batilda Salha Burian.
"Simba Terminal imetoa miche hii ya minazi kusaidia ukuaji uchumi Gombero, tunaomba kuendelea kushirikiana miche hii ikue ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kutimia"alisema Tirya.
Pamoja na hayo Tirya ameishukuru Serikali kwa ushirikiano iliouonesha kwenye utekelezaji zoezi hilo akimweleza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na viongozi waliochini yake kuwa mstari wa mbele katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Kichangani kata ya Gombero, Mhina Godfrey Mntambo aliishukuru serikali na kampuni ya Simba Terminal kufikisha fursa hiyo ya ugawaji miche ya minazi kwa wakulima waliopo kwenye eneo lao.
Alisema,hapo awali hali ya uchumi wa kanda yao ilitegemea kilimo cha zao la minazi ambalo lilikufa kupitia sababu mbalimbali na kwamba hivi sasa baada ya kupokea mbegu hizo wamejiwekea mikakati kuhakikisha wanarejesha zao hilo la kihistoria.
"Tumejiwekea mikakati baada ya kupokea miche yetu 600, miche 100 tutaipanda kwenye shamba la mfano na 100 tutaigawa kwa wananchi"alisema Mntambo huku akiahidi kusimamia kikamilifu upandaji wa miche hiyo.
Naye Juma Kasidi wa kijiji cha Jirini alirejea kuishukuru serikali na Simba Terminal huku akishauri kutafutwa kwa mbinu mahususi ya kuwakabili tembo wanaoharibu minazi.
"Tunashukuru kwa msaada huu, ila tunaomba kusaidiwa Tembo wanaoshambulia minazi na kuiua" alisema Kasidi wakati akiwasilisha Shukrani zake kwa Serikali.
Mwananchi mwingine Swalehe Rashid Kamando aliahidi kukitumia vizuri kipindi hiki cha mvua kupanda minazi hiyo, alisema zao hilo lilikuwa kiu yao kubwa akieleza kwamba kwenye eneo lake kuna wakulima 60 na kila mmoja atapata miche 10.
Mwanamama Zainabu Hussein mwenye shamba la ekari tano, alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa kuiona jamii ya wanawake akisema kwamba miche hiyo ya minazi imetoa matumaini ya kuimarisha Uchumi wao.
Katika zoezi hilo la ugawaji wa miche ya minazi ambalo pia afisa Kilimo kata ya Gombero Esther Robert alikuwepo, alikiri kupokea miche 5,000 ya minazi kutoka Simha Terminal akisema itasaidia uendelezaji wa zao hilo la biashara kwa wananchi.
Miche ya minazi ikiwa tayari kwa kugaiwa kwa wananchi.
Miche ikiandaliwa tayari kwa kugaiwa kwa wananchi.
Miche ikichukuliwa na wananchi kwa kutumia vyombo vya moto
Miche ikiwa tayari kwa kukabidhiwa wananchi.
Post Comment
No comments