MTOTO ANAYESUMBULIWA PUMU YA NGOZI NA MOYO MAISHA YAKE HATARINI
AOMBA MSAADA WA MILIONI TATU ZA MATIBABU
Hali ilivyo hivi sasa ya Mtoto Abubakar Tenda (10) anayesumbuliwa na maradhi ya pumu ya ngozi na moyo kwa zaidi ya miaka tisa.
........................................
Na Dotto Mwaibale, Dar
es Salaam
MAISHA ya Mtoto Abubakar
Rajab Tenda (10) ambaye kwa zaidi ya miaka tisa hajawahi kufurahia maisha na kuwa mdhoofu wakati wote kutokana na
maradhi ya moyo na pumu ya ngozi yanayomsumbua maisha yake yapo hatarini kwa kukosa
Sh. Milioni 3.2 za matibabu hivyo anaendelea kuwaomba watanzania wamsaidie.
Mama ya mtoto huyo Latifa
Saidi (37) mkazi wa Mtoni Mtongani jirani na Msikiti Mweupe Mtaa wa Mseti Temeke Jijini Dar es Salaam
anasema hana fedha za matibabu ya mwanaye huyo ambaye wakati wote iwe mchana, iwe usiku amekuwa akijikuna kwa kutokwa
upele mithiri ya magamba ya samaki huku akipata maumivu makali.
“Tumaini langu la kupata
matibabu ya Abubakar nawaachia watanzania kwani ndani ya kipindi cha miaka
tisa nimekuwa nikiangaika naye sehemu
mbalimbali kwa ajili ya matibabu nimeshindwa kupata kiasi hicho cha fedha kama
nilivyoambiwa na daktari wake,” alisema Latifa.
Latifa anasema mtoto
huyo hajawahi kupata usingizi na kuwafanya wawe wanakesha wakimuangalia jinsi
anavyojikuna na kuugulia maumivu.
Mama huyo anasema
alimzaa Abubakar Juni 10, 2014 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Jijini Dar
es Salaam akiwa na kilo 4.5 na kuwa alianza kuona mabadiliko ya mtoto wake alipofikisha miaka mitatu kwani ngozi yake ilianza kuonesha kutokwa na upele
ndipo alipo mpeleka Hospitali ya Bruda iliyopo Kijichi lakini hakupata nafuu.
Latifa anasema
aliendelea kumtibu katika hospitali mbalimbali na alipofikisha miaka sita akawa
anapata joto kali nyakati za usiku, kukooa na uso kuvimba ndipo alipompeleka
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke walimuambia alikuwa na changamoto
ya moyo hivyo ampeleke Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya
matibabu.
Alisema baada ya
kufanyiwa vipimo alielezwa kuwa moyo wake umetanuka hivyo anatakiwa kufanyiwa
upasuaji kwa gharama ya Sh. Milioni 3.2 fedha ambazo ameshindwa kuzipata jambo
linalomfanya mtoto wake huyo aendelee kuteseka na kushindwa kuanza shule.
“Kwa kweli sijui hatima
ya mwanangu kwani wakati wote hana furaha na sijui nitapata wapi hizo fedha
sina na mume wangu naye hana kazi ya
uhakika hivyo kutuwia vigumu namna ya kupata fedha hizo,” alisema Latifa.
Alisema mwezi uliopita
ndio ilikuwa ampeleke kliniki lakini hadi leo hii ameshindwa kufanya hivyo
kwani kila inapofika tarehe ya kliniki anatakiwa awe na Sh. 120,000 kwa ajili
ya vipimo na mahitaji mengine ya chakula na usafiri fedha ambayo hana kwani
hata kodi ya nyumba ambayo ni zaidi ya Sh.250,000 ameshindwa kulipa hivyo
ametakiwa aondoke kwenye nyumba hiyo na kumfanya hazidi kuchanganyikiwa na kuona dunia kama imemtupa.
“Sina mbele wala nyuma
sijui nitazimaliza vipi hizi changamoto nilizonazo nawaombeni watanzania
wenzangu kwa umoja wenu mnisaidie matibabu ya mtoto wangu,” alisema Latifa akionesha kukata tamaa kabisa ya maisha.
Ndugu zangu watanzania mmeyasikia
madhira yanayomsibu mtoto huyo pamoja na changamoto alizonazo mama yake Latifa
Saidi anaomba msaada wetu kwa chochote kile utakachoweza kumsaidia kwake
kitakuwa ni kikubwa kwani kuna usemi wa Kiswahili unaosema haba na haba ujaza
kibaba lengo ni zipatikane fedha za matibabu ya mtoto wake huyo.
Kwa atakaye kuwa tayari
kumsaidia mtoto huyo hata kwa Sh. 2000 ana weza kuwasiliana na mama yake moja kwa moja kwa namba ya simu 0788034472 au
Mwandishi wa taarifa hii kwa namba 0754362990.
Taarifa hii nimelazimika kuirudia kuiandika kwa mara ya pili baada ya Juni 6, 2025 kwenda kumjulia hali mtoto huyo na kumkuta akiwa katika hali isiyoridhisha kwani hivi sasa anashindwa kutembea vizuri huku upele ukiendelea kusambaa mwili mzima na mapigo ya moyo yakipanda kwa nguvu, shime watanzania kila mmoja kwa uwezo na imani yake tuungane kwa pamoja kuokoa maisha ya mtoto huyu anayepitia wakati mgumu kwa kukosa Sh. Milioni 3.2 za matibabu.
Latifa Said, akiwa na mtoto wake nyumbani kwao wanakoishi Mtoni Mtongani
Post Comment
No comments